Sasa hakuna longolongo tena, Yanga imeishamalizana na Kocha Marcio Maximo ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili.
Ingawa unaweza kusema hii ni kufuru, kwani tayari Yanga imefanikiwa
kumsainisha Marcio Maximo mkataba wa miaka miwili na anatua nchi kesho saa saba
7:55 mchana tayari kuanza kazi.
Maana yake kuanzia leo, hesabu saa 24 wakati Wabrazil hao
watatu watakapotua Yanga ambayo inaweka rekodi mpya ya kuajiri Wabrazil watatu
kwa wakati mmoja.
Maximo hatakuwa peke yake, anatua akiwa na msaidizi wake,
Leonardo Neiva Martins ambaye pia amesaini mkataba wa kuifundisha Yanga kwa
miaka miwili pia wataongozana na kiungo mshambuliaji mmoja aitwaye Andrey
Ferreira Coutinho.
Watatu hao watatua kwenye Uwanja wa Ndege wa Johannesburg
nchini Afrika Kusini, alifajiri na wataondoka hapo saa 3:30 asubuhi kuja jijini
Dar es Salaam.
Mshambuliaji huyo ambaye Maximo amewaambia Yanga kuwa ni
tishio anayeweza mikiki ndiye chaguo lake baada ya kuambiwa aje na mchezaji
mmoja ambaye aanaamini atakuwa msaada kwa Yanga na kwake pia.
Watatu wote hao watatua nchini wakiwa ndani ya dege la
Shirika la Ndege la Afrika Kusini maarufu kama SAA na mara moja watapelekwa
kupumzika kabla ya siku inayofuata kukutana na Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji.
SALEHJEMBE kilikuwa chombo cha habari cha kwanza nchini kwa upande wa mtandao kueleza kuhusiana na ujio huo wa Maximo ambaye mara ya kwanza aliichoropoka
Yanga kidogo tu na nafasi yake ikachukuliwa na Ernie Brandts raia wa Uholanzi.
Hadi anatua Yanga, Coutinho alikuwa anakipiga katika klabu ya
Pysandu inayoshiriki Ligi Darala la Pili nchini Brazil maarufu kama Serie C.
Amezaliwa Januari 12, 1990, maana yake ana umri wa miaka 24
na ameahidi kuonyesha uwezo mkubwa ili iwe nafasi kwake kusonga mbele zaidi ya
hapa Tanzania.
Hata hivyo, Coutinho alikuwa ameichezea Pysandu mechi tatu tu
dhidi ya Luverdense, Araguaina na Rio Branco-AC.
Hata hivyo, Yanga haitakuwa klabu ya kwanza kuleta mchezaji
rais wa Brazil, moja wapo ni Coastal Union iliyofanya hivyo msimu uliopita,
lakini mchezaji huyo akashindwa na kurejea kwao huku akisisitiza mazoezi
yalikuwa makali kama ya riadha.
Lakini inawezekana Coutinho akawa na nafasi nzuri ya kucheza
kwa kuwa atakuwa chini ya Wabrazil wawili ambao wanaujua uwezo wake.
Neiva ambaye ni msaidizi, moja kwa moja anachukua nafasi ya
Mkwasa ambaye amepata kazi nchini Saudi Arabia na sasa atainoa Shaolah FC akiwa
chini ya Hans van der Pluijm aliyekuwa bosi wake Yanga.
0 COMMENTS:
Post a Comment