Kocha Mkuu wa
Serengeti Boys, Hababuu Ali Omari amesema morali ya wachezaji wake ipo juu kwa
ajili ya mechi dhidi ya Afrika Kusini (Amajimbos) itakayochezwa kesho (Julai 18
mwaka huu).
Mechi hiyo ya
kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya
miaka 17 itafanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es
Salaam kuanzia saa 10 jioni.
Akizungumza kwenye
mkutano na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF jijini Dar es Salaam leo,
Kocha Hababuu amesema nia ya kikosi chake ni kuhakikisha wanafika kwenye
fainali za Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Niger.
“Tunaiheshimu
Afrika Kusini, lakini hatuiogopi. Morali ya wachezaji ipo juu na wanajiamini.
Kimsingi wanajua kuwa hii ndiyo njia ya wao kutokea kwenye mpira wa miguu, kwa
hiyo lengo ni kushinda,” amesema Kocha Hababuu.
Naye Kocha wa
Afrika Kusini, Molefi Ntseki amesema anaziheshimu timu za Tanzania, na
changamoto aliyonayo ni kuhakikisha kuwa anashinda mechi hiyo kwani mara ya
mwisho kwa timu yake kushiriki fainali za Afrika ilikuwa miaka sita iliyopita.
Kiingilio katika mechi hiyo ni sh. 2,000 na tiketi
zitapatikana uwanjani kwenye magari maalumu.
0 COMMENTS:
Post a Comment