Katibu Mkuu wa Coastal
Union, Kassim El Siagi atafikishwa kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) kwa kushinikiza mkutano wa wanachama wa klabu
hiyo ufanyike bila kuandaliwa na Kamati ya Utendaji.
Pia El Siagi alitumia
vyombo vya habari kuishambulia TFF ambayo haikutambua uamuzi wa mkutano huo
ulioelezwa kumdumaza Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Steven Mnguto.
TFF ilimtuma
Mkurugenzi wake Msaidizi wa Sheria na Uanachama kufanya uchunguzi wa mgogoro
uliokuwa unaendelea katika klabu hiyo.
Baada ya kupokea
taarifa ya uchunguzi huo, TFF imebaini kuwa Mwenyekiti na Mweka Hazina wa klabu
hiyo walishajiuzulu, hivyo uitishwe uchaguzi haraka na kujaza nafasi hizo na
nyingine zilizo wazi.
Pia wajumbe wa Kamati
ya Utendaji ya Coastal Union, Salim Amir na Albert Peter wameonywa kwa
kushiriki katika mkutano ambao wanajua haukuandaliwa na Kamati ya Utendaji.
Vilevile uchunguzi wa
TFF umebaini kuwa ushiriki wa Salim Bawazir na Akida Machai kwenye vikao vya
Kamati ya Utendaji ya Coastal Union si halali kwa vile wajumbe wa kamati hiyo
wanachaguliwa na Mkutano Mkuu na si kuteuliwa na Mwenyekiti.
Kwa vile kutakuwa na
uchaguzi wa kujaza nafasi ambazo zipo wazi, uchaguzi huo utasimamiwa na Kamati
ya Uchaguzi ya Coastal Union kwa kushirikiana na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, na
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tanga na Coastal Union watafanya uhakiki wa
reja ya wanachama.
0 COMMENTS:
Post a Comment