EMERSON |
Na Saleh Ally
YANGA imemleta kiungo
Emerson Roque ambaye tulielezwa amekuja kwa ajili ya kufanya majaribio ya wiki
moja hadi mbili.
Amefanya kwa siku tatu,
benchi la ufundi la Yanga limetangaza kuridhishwa na kiwango chake na baada ya
hapo amepewa mkataba wa mwaka mmoja.
Majaribio ya siku nne! Tena
Yanga ikiwa inafanya mazoezi ya kukimbia, hajapewa hata mechi? Kwa maelezo ya
mwanzo ya uongozi wa Yanga, kidogo inashangaza!
Lakini kwa maana ya hali
halisi, uwezo wa kiungo yule kupitia video inayoonyesha mechi zake mbalimbali,
anastahili kupewa mkataba. Lakini kwa nini sasa uongozi ulisema unamfanyia
majaribio?
Simba nao wamemleta kijana
Omar Mboob raia wa Gambia ambaye wengine walisema anatokea Gabon. Kijana huyo
tayari yuko nchini, ameanza majaribio na Simba, wamesema atakuwa nchini kwa
wiki mbili.
Hatujajua kama Simba nao
watakwenda kwa njia ileile waliyopita Yanga, ya kusema anafanya majaribio
halafu Mgambia huyo apewe mkataba ndani ya siku tano tu kwa madai benchi
limeridhika wakati majaribio yalikuwa ni ya danadana bila hata mechi!
Lengo si kukosoa Simba au
Yanga walivyofanya, kwanza ni kueleza kwamba walichokifanya si utaratibu mzuri
wa kuwajaribu wachezaji. Vizuri zaidi, wangekaa kimya tu bila ya kutangaza ni
majaribio.
Muhimu hasa ni suala la
nini klabu zinaingiza, nini zinatoa hasa katika suala la gharama. Ndiyo maana
naangalia kama kweli usajili wa wachezaji kutoka nje unakuwa ni muhimu au
fasheni tu.
Yanga na Simba zimekuwa
zikihaha kulazimika kuongeza fungu la fedha ili kukamilisha mishahara ya mwezi
ya wachezaji. Bia ya Kilimanjaro ambayo ni mdhamini wao, inatoa kipande cha
mshahara.
Mshahara wanaotoa
Kilimanjaro, kama ungepelekwa Mtibwa Sugar, Kagera Sugar au timu nyingine
ambayo si Yanga, Azam FC au Simba, ungetosha vizuri sana.
Msisitizo ni kwamba,
mishahara kwa timu kongwe za Yanga na Simba, unakuwa juu sana kutokana na
gharama ya juu wanaolipwa wageni kama akina Emerson na wenzake. Je, wana
tofauti kubwa sana na wachezaji wa hapa nyumbani?
Wakati Simba na Yanga
zinagharimia wageni kwa kiasi kikubwa, zinajua kwamba zinacheza na hasara bila
ya sababu za msingi.
Mfano, Simba inaonekana
isingehitaji kuongeza mchezaji wa kigeni katika kipindi hiki ili kubana
matumizi kwa kuwa haina michuano ya kimataifa na kuna uwezekano wa kupata kiungo
bora hapa nyumbani kama kutakuwa na uchambuzi wa kutosha kutafuta kiungo bora.
Mimi ninaona Yanga na Simba
zinapata hasara kubwa kutokana na gharama za matumizi ukilinganisha na kipato
chao kwa wakati huu. Sababu hizi hapa.
Mechi:
Mechi za ligi ni nne tu kwa
mwezi, moja kwa kila wiki. Maana yake wachezaji wanaweza kuitumikia timu na
kuingiza fedha kwenye klabu mara nne tu kwa mwezi.
Hii inatokana na ratiba ya
ligi kuwa kila timu inacheza mara moja kwa wiki.
Hakuna anayeweza kukataa
kuwa soka ni biashara, timu inatakiwa kushinda ili kuongeza imani kwa mashabiki
wake ili wajitokeze kwa wingi uwanjani. Lakini inaposhinda na kufanikiwa kubeba
kombe au nafasi ya pili, inashiriki michuano ya kimataifa na kuingiza fedha
zaidi kama itafanya vizuri.
Kwa misimu miwili, Simba
imekuwa na wachezaji wa kimataifa, haikushika hata nafasi ya pili. Hii inaonyesha
kuna tatizo, pia inathibitisha wachezaji wa nyumbani wakipewa nafasi, wnaweza
wakafanya vizuri na kusaidia kupunguza gharama kama zile za kuwasafirisha wachezaji
wa nje, kulipia vibali vya kufanya kazi nchini na kadhalika.
Azam TV:
Kuonyeshwa moja kwa moja
kwa mechi kupitia Azam TV, bado ni tatizo kwa timu hizo mbili kubwa, kwani
watazamaji wanapungua kwa wingi viwanjani.
Sh milioni 100 inayotolewa
na Azam TV kwa msimu, bado haitoshi kwa Yanga na Simba ambazo zinaweza
zikaingiza fedha kama hizo katika mechi moja tu.
Hakuna ubishi kama ambavyo
Yanga walikuwa wakidai, timu hizo mbili ndizo zinazovuta watu wengi zaidi.
Kweli zilistahili kulipwa zaidi ya nyingine na ilikuwa ni haki, lakini kwa
fedha zinazopata sasa, si sahihi.
Suluhisho:
Kupunguza ukubwa wa hasara
kila kukicha, Yanga na Simba zinapaswa kuangalia suala la kutumia wachezaji
wengi zaidi wa nyumbani,
kwani wachezaji wengi
wanaoletwa wanakuwa hawana viwango tofauti sana na wale wa hapa nyumbani.
Bado naendelea kupinga
kusema Hamisi Kiiza wa Yanga, ana tofauti kubwa na Mussa Hassan Mgosi ambaye
anamzidi umri.
Iwapo timu hizo zitaendelea
kukubali kuangalia ushabiki, kujaza wachezaji wa kigeni rundo huku zikiendelea
kulimbikiza madeni kutoka kwa wadau au wanachama wake, haitakuwa sahihi.
Deni kila linavyozidi
kupanda, huongeza presha au kuvuruga uhusiano kati ya pande mbili
zilizokubaliana. Kwa urahisi zaidi, iko haja ya kuwa na timu imara na makini za
kusaka, kufufua na kuviendeleza vipaji hapahapa nyumbani, inawezekana kabisa.
Huwa nashindwa kuelewa mada zenu, kwa miaka ya karibuni ni mchezaji gani wa Tanzania ambaye amekuwa mfungaji bora angalau kwa miaka miwili mfululizo!? Unamzungumzia Mgosi, hivi kwanini kama yeye ni bora hayuko Azam, Yanga wala Simba!? Tatizo la wachezaji wa kibongo hawajitambui na hawana malengo. Mtu kama Samata na Ulimwengu ni mfano wa kuigwa Tanzania. Muangalie leo chuji, kila siku anajisifia hakuna midle kama yeye bongo na mimi nakubali, lakini hajitambui sasa wanini kwenye club!? huwezi kulinganisha Simba/Yanga/Azam na Mtibwa, wakati mtibwa anacheza ili ashike nafasi za juuu wenzake wanaangalia ubingwa na mechi za kimataifa.
ReplyDelete