Uongozi wa Klabu ya Yanga
umefunguka kuwa unasubiria kuona Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), litachukua
hatua gani kutokana na kitendo cha mshambuliaji wake Amissi Tambwe kukabwa koo
na mchezaji wa Ruvu Shooting.
Tambwe alichezewa rafu
kadhaa na beki wa timu hiyo, George Michael, mpaka akachanika mdomoni lakini
mwamuzi hakuchukua hatua yoyote.
Katika mchezo wa Jumamosi
kati ya Yanga na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa, kulikuwa na vurugu kiasi
cha kufikia hatua mechi kusimama mara kwa mara.
Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha, amefunguka kuwa wamesikitishwa na kitendo kilichotokea katika
mchezo huo na kudai kuwa kuna matukio mengi ambayo hayakuwa sawa, hivyo
wanawasubiri TFF kuona watachukua hatua gani kuhusiana na suala hilo.
“Hatukutaka kulizungumzia
suala hili kwa watu na tulihitaji Watanzania waone wenyewe kama picha
ilivyojieleza kwenye magazeti (anamaanisha Championi).
“Tunasubiri watu wenye
dhamana ya mpira tuone watatoa maamuzi gani kuhusiana na mechi hiyo, kwani
matukio mengi ambayo siyo mazuri yalijitokeza katika mchezo ule.
“Nadhani waamuzi wataandika
ripoti yao, kamisaa wa mchezo pia ataandika na kila mmoja ameona, hivyo
tunasubiri maamuzi yatakuwaje kwani kitendo kilichofanywa siyo kizuri na iwapo
hakuna hatua watakayochukua tutajua cha kufanya,” alisema Tiboroha.
Alimalizia kwa kusema lengo
ni kuhakikisha wachezaji wao wanakuwa na usalama kwa kutopatwa na matatizo.
0 COMMENTS:
Post a Comment