Kikosi cha wachezaji nyota wa zamani wa Barcelona FC kinatarajia kushuka nchini kucheza dhidi ya wachezaji wa zamani
wa Tanzania, Tanzania All Stars Machi 28 kwenye uwanja wa Taifa jijini.
Mwakilishi
wa wachezaji wa zamani wa Barcelona, Patrick Kluivert alisema jana kuwa mechi
hiyo itawahusisha wachezaji nyota wa Barcelona wakiwemo, Edgar Davids, Gaiza
Mandieta, Ludovic Giuly, Francesco Coco na wengine wengi waliopitia klabu hiyo
kwa miaka tofauti.
Kluivert ambaye ni mchezaji nyota wa zamani wa Barcelona alisema kuwa kikosi chao kina wachezaji nyota ambao ni maarufu duniani na
wanaamini mechi itakuwa nzuri na yenye ushindani mkubwa.
Alisema
kuwa yeye ni mwenyeji sana hapa Tanzania kwani huu ni ujio wake wa tatu na
anaamini kuwa jinsi mashabiki wanapenda sana mpira wa miguu, itakuwa fursa
kubwa kwao kuona vipaji vya zamani ambavyo vimetukuka.
“Ninafurahi
kuja nchini Tanzania kwa mara ya tatu, ni faraja kubwa pia kucheza hapa nchini
kwa mara ya kwanza, naomba mashabiki wa soka wajae uwanjani kuona mpira wenye
ushindani,” alisema Kluivert.
Mwakilishi
wa kampuni ya Prime Time Promotion inayoratibu mechi na ziara ya timu hiyo ya
Barcelona, Stuart Kambona alisema kuwa madhumuni ya mchezo huo ni kudumisha
mahusiano ya kibiashara ya mpira wa miguu baina ya Tanzania na Hispania,
kutangaza utalii na kuendeleza mahusiano mazuri baina ya nchi hizo mbili.
Kambona
alisema kuwa pamoja na kucheza soka siku hiyo, ujio wao pia utaitangaza nchi
nje ya mipaka yake na kuleta fursa nyingi hapa nchini.
“Wachezaji
wa Barcelona wanataingia nchini siku mbili kabla ya mechi na watakuwa zaidi ya
20, majina ya wachezaji wengine yatatangazwa baadaye, ila tunaomba wadhamini
wajitokeze kufanikisha na kufaidika na mechi hiyo,” alisema Kambona.
Mwenyekiti
wa Chama cha soka cha mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) Almasi Kasongo
aliwaomba mashabiki wa soka kujiandaa kuangalia mechi hiyo kwa kufika
uwanjani.
Kasongo
alisema kuwa DRFA imefarijika sana kwa ziara hiyo na kuiomba Prime Time
Promotion kuhakikisha kuwa inapanua wigo kwa kuandaa mechi nyingi ambazo
zitakuwa chachu ya maendeleo ya soka nchini.
0 COMMENTS:
Post a Comment