February 4, 2015



Na Saleh Ally
YANGA inacheza mechi yake ya 12 ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, leo.


Baada ya hapo, itakuwa imebakiza mechi moja ya kiporo dhidi ya Mbeya City. Bado Yanga iko kwenye presha kwa kuwa mambo hayaendi vizuri.

Wakati Kocha Marcio Maximo anaondoka, ilionekana mbadala wake si zaidi ya Hans van der Pluijm ambaye alikuwa ameiacha Yanga na kwenda kujiunga na Al Shaolah FC ya Saudi Arabia.


Kweli, uongozi ulifanikiwa kumrudisha kocha huyo kipa wa zamani wa timu ya taifa ya Uholanzi na msaidizi wake, Charles Boniface Mkwasa.

Pamoja na makocha, Yanga imefanya mabadiliko makubwa katika safu ya ushambuliaji ikiwa ni pamoja na kusajili mafowadi wapya watatu.

Wawili kutoka nje ya Tanzania, Kpah Sherman raia wa Liberia na Amissi Tambwe wa Burundi. Halafu mzoefu, Danny Mrwanda. Utaona walionyesha makali yao katika mechi za Kombe la Mapinduzi huko Zanzibar.

Kwa uwezo wa Pluijm na Mkwasa, uzoefu wa Tambwe, Sherman na Mrwanda, Yanga wana kila sababu ya kuwa na matumaini makubwa ya kuona kikosi chao kinafanya vema katika ligi.


Ukiachana na hao, Yanga ina wakali wengine wenye uwezo wa ‘kusema’ na nyavu na wamekuwa wakicheza. Mrisho Ngassa na Simon Msuva.

Bado kuna wawili walio benchi lakini uwezo mkubwa wa upachikaji mabao unajulikana. Angalia Jerry Tegete pia Hussein Javu ambao kama watacheza katika timu nyingine wakapata nafasi ya kutosha, wana kila sababu ya kung’ara.

Sasa tatizo lipi hasa Yanga? Ukiangalia mechi zao utagundua mambo kadhaa lakini kinachoonekana kwa haraka ni upotezaji kupindukia wa nafasi za kufunga mabao.


Katika mechi ya mwisho ya Yanga ilipokutana na Ndanda FC kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, tuliona namna nafasi nyingi za kufunga zilivyopotea.

Tambwe nafasi tatu, Sherman mbili kama ilivyo kwa Msuva, Mrwanda pia moja. Hilo ndiyo tatizo namba moja na linahitaji ufumbuzi wa haraka.

Nani anahitaji kulijibu? Tambwe, Sherman, Ngassa, Msuva, Mrwanda lakini hata Tegete na Javu wakipata nafasi, nao wanaweza kueleza jambo.

Kwa kupitia mfumo wa Pluijm na Mkwasa, tumeona wazi Yanga imekuwa ikitengeneza nafasi za kutosha za kufunga mabao na kinachobakia ni washambuliaji kugusa kwa kichwa, mguu na hata ikiwezekana kwa kifua ili kuandika bao.

Ajabu inashindikana! Katika soka kukosa nafasi ni jambo linalotokea lakini mshambuliaji bora ni yule mwenye uwezo wa kutumia nafasi kuanzia asilimia 75 na kukosa chache. Anayekosa 75% na kupata chache hawezi kuwa bora.

Mechi ya dakika 90, timu bora inaweza kutengeneza nafasi za uhakika za kufunga sita hadi kumi. Au ubora wa kiwango kwa siku na makosa mengi ya kiungo na difensi ya safu ya ulinzi yanaweza kuifanya timu moja ikatengeneza hadi nafasi 20.

Sasa Yanga kama imeweza kutengeneza hadi nafasi 10 nzuri za kufunga, vipi inashindwa kufunga hata mabao matatu? Jiulize ni sahihi kuona Pluijm anakosea?

Lazima Tambwe, Sherman, Mrwanda, Msuva na wengine wawe na majibu ya hilo ingawa wana kila sababu ya kujifunza jambo moja, presha.

Wakikubali hofu au presha iwatawale kutokana na hali ilivyo na mashabiki wanavyolalamika, huenda wakapotea kabisa.

Uwezo wa kufunga kwa Ngassa, Msuva, Sherman, Tambwe na wengine wala si jambo jipya, inajulikana wanaweza. Sasa mbona hawafungi? Wameshindwa kuwa bora.

Wameshindwa kuwa bora kwenye kutumia nafasi, lakini wameshindwa kuwa bora kuidhibiti presha ambayo sasa inawatafuna. Mchezaji mzoefu hurekebisha mambo kwa kupambana na presha na ndilo jambo wanaloweza kulifanya dhidi ya Coastal, leo.

Iwapo Yanga watashinda leo au kufunga mabao mawili au matatu, basi wanaweza kurejesha hali ya kujiamini na ikiwezekana mechi nyingi zinazofuatia wakafunga mabao mengi zaidi na kuwa kweli safu bora au tishio ya ufungaji maana kwa sasa bado ni majina tu!

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic