SIMBA
imeshinda bao 1-0 dhidi ya Yanga katika mchezo safi wa Ligi Kuu Bara uliopigwa
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, jana.
Mchezo huo
ulikuwa mtamu na wa kuvutia, kila timu ilionyesha kiwango kizuri ingawa baadhi
ya wachezaji walishindwa kuonekana kama ilivyokuwa imetakiwa. Kuna mengi
yanaweza yanajitokeza katika mechi ya watani kama hiyo.
Achana na
vituko, lakini utaona tofauti ya wachezaji hata wale uliokuwa unawategemea
watang’ara wameshindwa kabisa kuonyesha viwango vyao kama ilivyozoeleka.
Lakini kuna
wale ambao uliona hawawezi kuwa tishio ndiyo wamefanya kile ambacho wengi
hawakukitegemea na ndiyo maana ya mechi ya watani, ni mechi ya mambo mengi.
Unalizungumzia
bao lililomaliza mechi hiyo lililofungwa na Emmanuel Okwi baada ya kupiga mpira
ambao uliokuwa si lahisi kudhaniwa ungeweza kuingia kwenye lango la Yanga.
Bao hilo
limekuwa jibu sahihi la maswali mengi ya siku kadhaa kuhusiana na mechi hiyo ya
watani ambayo kabla haijachezwa kunakuwa na maswali milioni watu wakijiuliza na
kujijibu.
Wako ambao
wamekuwa wakitabiri, wako ambao wamekuwa wakifanya ushirikina, wako ambao
wamekuwa wakishikana uchawi na mwisho kuzozana, lakini shuti moja la ufundi
kabisa la Okwi limetoa jibu la maswali zaidi ya mia watu waliokuwa wakijiuliza.
Ushirikina
hutawala katika mechi ya watani, kusingiziana, watu kuhisi na kuziamini hisia
zao ni sehemu ya mambo ambayo yamekuwa yakitawala katika mechi hiyo.
Wachezaji
wanapewa huduma nzuri za kulala hoteli ambazo hawawezi kulala wanapokuwa
wanakutana na Kagera Sugar au Ndanda FC. Lakini mwisho, bao la Okwi, limekuwa
jibu sahihi.
Huenda huu
ndiyo wakati mzuri pia kwa mashabiki wa soka nchini na wale wajanjawajanja
ndani ya klabu za Yanga na Simba ambao wamekuwa wakisema wanakwenda kuroga,
wapate jibu.
Bao la Okwi
halina uchawi, bao la Okwi si la kishirikisha, mguu wake aliopiga si mguu wa
shetani, badala yake kuna mambo matatu muhimu ambayo yakipewa nafasi yanaweza
kuendeleza soka na wala si ushirikina.
Okwi ana
kipaji, Okwi alikuwa mjanja kwa mawasiliano kati ya ubongo kupitia macho na
baadaye kuamua kwa mguu. Lakini tatu, lazima tukubali juhudi aliyoifanya
kutokana na kuwa fiti yaani mazoezi ndiyo lilikuwa jibu la uwezo wa kumaliza
kazi aliyoifanya.
Wakati mzuri
wa kuacha kuamini mambo ya kishirikina na kuheshimu kuwa mpira una mambo yake
muhimu kwa ajili ya kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri.
Ushirikina
katika soka hauna msaada, ni miradi ya wachache ndani ya klabu ambao wamekuwa
wakisema wana mapenzi na klabu hizo, kumbe wanazipenda kwa kuwa zinawapa
chochote kitu cha kuendesha maisha yao.
Kama upande
wa Yanga walikwenda kufanya ushirikina vipi hawakufunga, hata Simba mbona
hakuna bao la kishirikina na badala yake tumeona sayansi ya Okwi ilivyofanya
kazi waziwazi? Vizuri kuachana na hisia duni ili kuepuka kuwa watu duni
tusiokwenda na kasi ya maendeleo ya dunia.
Kingine cha
nyongeza ni kusaka wachawi. Huu ndiyo utakuwa wakati wa Yanga kuanza kutangaza
fulani na fulani ni tatizo au walihongwa. Bao alilofungwa Barthez, angefungwa
yoyote kwa kuwa akili nyingi za Okwi zilikuwa za haraka kuliko kawaida.
Unaweza
kidogo ukalifananisha na bao la Jaja raia wa Brazil aliyeifungia Yanga
ikipambana na Azam FC. Lakini la Okwi, limekuwa bora zaidi kutokana na
lilivyotokea. Hivyo soka ina mambo yake, Yanga wakubali wamepoteza waangalie
mbele na si kuanza kupambana na kuvurugana.
0 COMMENTS:
Post a Comment