Uongozi wa Yanga umetamka kuwa, hauna
mpango wa kuachana na mchezaji wao, Said Bahanuzi, anayeichezea Polisi Moro kwa
mkopo kutokana na uwezo alionao na kiwango kikubwa anachokionyesha kwa sasa.
Bahanuzi ambaye alikuwa na maisha ya
benchi Yanga, kwa sasa anang’ara na Polisi Moro baada ya kuwa msaada mkubwa kwa
timu hiyo katika safu ya ushambuliaji na kufanikiwa kuifungia mabao matatu
mpaka sasa.
Hata hivyo, Bahanuzi amebakiza miezi
michache kumaliza mkataba wake Yanga na tayari kuna taarifa kuwa baadhi ya timu
zimeanza kunyemelea saini yake, hivyo Yanga wameibuka na kuweka wazi misimamo
yao hiyo na mchezaji wao huyo kupitia kwa katibu wake, Jonas Tiboroha ambapo
alifafanua kuwa hawapo tayari kumuachia kirahisi mshambuliaji huyo wa zamani wa
Mtibwa Sugar.
“Bahanuzi ni mmoja wa wachezaji waliopo
kwenye mipango ya benchi la ufundi mpaka sasa na tumemtoa kwa mkopo kwa ajili
ya kwenda kuongeza baadhi ya vitu ili msimu ujao akirudi tuweze kumtumia
kikamilifu, kwa hiyo bado tunamhitaji, hatupo tayari kumuachia mchezaji kama
huyo kama timu nyingine zinavyodhani,” alisema Dk Tiboroha.
Pamoja na hayo, taarifa zaidi
zinaeleza kuwa, moja ya timu zilizopo kwenye mipango ya kumnyakua straika huyo
ni mahasimu wa Yanga, Simba SC.
0 COMMENTS:
Post a Comment