Kivumbi na jasho cha Ligi Kuu Bara
kinatarajia kuendelea tena leo katika viwanja vinne tofauti lakini mechi
inayotupiwa macho zaidi na wapenzi wa soka hapa nchini ni ile ya Simba na
Mtibwa Sugar itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mechi hiyo inatarajiwa kuwa
na ushindani mkubwa kutokana na rekodi mbalimbali za timu hizo msimu huu ambapo
katika mchezo wa kwanza uliozikutanisha mjini Morogoro, zilitoka sare ya bao
1-1 na hata kwenye fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyofanyika visiwani
Zanzibar, Simba ilishinda kwa penalti 8-7.
Kikosi cha Simba kinachofundishwa
na Mserbia, Goran Kopunovic, kitashuka katika mechi hiyo kikiwa na kumbukumbu
ya kushinda michezo miwili iliyopita ambayo ni dhidi ya Prisons (5-0) na Yanga
(1-0).
Simba sasa hivi wapo nafasi
ya tatu kwenye msimamo wakiwa na alama 26 huku Mtibwa wakiwa na pointi 23,
nafasi ya tano.
Kopunovic ameliambia Championi
Jumamosi kuwa, wataingia uwanjani wakiwa na kazi moja tu ya kuhakikisha wanapata
ushindi huku pia akilia kumkosa mshambuliaji wake, Ibrahim Ajibu ambaye
anatumikia kadi tatu za njano.
“Itakuwa ni mechi ngumu kwani
Mtibwa Sugar siyo timu mbaya lakini nimeshawaandaa vijana wangu kiufundi na kisaikolojia
kuhakikisha wanapambana ili tuweze kupata ushindi.”
Naye Kocha Mkuu wa Mtibwa
Sugar, Mecky Maxime, alisema: “Sina mengi ya kuongea juu ya mechi hiyo ila
jambo la msingi ni kwamba tutaingia uwanjani kupambana ili tuweze kuibuka na
ushindi kwani na sisi tunazihitaji hizo pointi tatu.”
Mechi nyingine
zitakazochezwa leo ni Prisons dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Sokoine,
Ruvu Shooting itapambana na Coastal Union (Mabatini) na Polisi Moro
itakabiliana na JKT Ruvu (Jamhuri).







0 COMMENTS:
Post a Comment