Na
Saleh Ally
KAMA
utakuwa mfuatiliaji wa mambo, hakika utakuwa umeona kazi safi na ya kuvutia ya
mshambuliaji Carlos Arturo Bacca Ahumada anayekipiga katika kikosi cha Sevilla.
Sevilla
sasa ndiyo mabingwa wa Ligi ya Europa kwa miaka miwili mfululizo, lakini
wakiweka rekodi ya kubeba kombe hilo mara nne katika miaka tisa.
Katika
kuutwaa ubingwa huo mara mbili mfululizo, huwezi ukatoa pongezi bila
kumzungumzia mshambuliaji huyo hatari mwenye sura kama vile hawezi kabisa
kucheza soka.
Bacca
ndiye amekuwa chachu ya mabadiliko makubwa ya ukali wa safu ya ushambuliaji ya
Sevilla ambayo imemaliza La Liga ikiwa katika nafasi ya tano baada ya mabingwa
Barcelona, Madrid katika nafasi ya pili, pia Atletico Madrid na Valencia.
Kwa
ufungaji mabao akiwa na 20, Bacca pia yumo katika tano bora baada ya kinara
Cristiano Ronaldo (48), Lionel Messi (43), Antoine Griezman (22) na Neymar
(22).
Asili
ya Bacca ni nchini Colombia, mchezaji ambaye alianza kusaka maisha yake akiwa
konda wa daladala katika mji aliozaliwa wa Puerto Colombia nchini Colombia.
Bacca,
28, aliishi maisha ya shida sana huku mpira ukiwa ni sehemu ya maisha yake
lakini alishindwa kushiriki vya kutosha kutokana na ugumu wa kazi yake ya ukondakta
aliyokuwa akiifanya.
Wakala
mmoja ndiye aliyempeleka katika kikosi cha Atletico Junior huku akimuahidi
atakuwa akimlipa fedha alizokuwa akipata kutokana na ukondakta. Alifanya hivyo
baada ya kuona uwezo wake mkubwa wa kufunga mabao.
Bacca
anaaminika ni mmoja wa wachezaji watano wabunifu zaidi duniani akiungana na
Eden Hazard, Messi, Neymar na Ronaldo katika kundi la wachezaji wenye uwezo
mkubwa wa kufunga na kutengeneza mabao.
Raia
huyo wa Colombia aliishi maisha magumu sana, taarifa zinaeleza hata kupata
mpenzi ilikuwa kazi kubwa kutokana na muonekano wake kama mtu mzima licha ya
kwamba alikuwa na umri mdogo.
Karibu
kila timu aliyoichezea katika maisha yake, ameibuka kuwa mfungaji bora wa
kikosi hicho. Alitua barani Ulaya kwa mara ya kwanza mwaka 2012 na kuichezea St
Bruges ya Ubelgiji ambako aliibuka mfungaji bora na mwaka uliofuata akajiunga
na Sevilla.
Sevilla
ambayo ilimsajili kwa euro milioni 7, imefaidika kwa kiasi kikubwa na
mshambuliaji huyo asiyependa makuu na mjanja kweli akiziona nyavu mbele yake.
Kwa
sasa ndiye anayepewa nafasi ya kuchukua mikoba ya Radamel Falcao katika kikosi
cha Colombia na inaonekana yu tayari baada ya kuwa na mchezo mzuri katika mechi
ya Kombe la Dunia dhidi ya Brazil nchini Brazil.
Konda
huyo wa zamani nchini Colombia, sasa ndiye staa wa nchi hiyo na tabia yake ya
utaratibu imemfanya awe kivutio zaidi kwa mashabiki wengi wa soka wa nchi hiyo.
Huenda
kwa kuwa hajacheza Madrid au Barcelona, kumekuwa na ugumu kidogo kumsikia kila
mara. Bacca ni mmoja wa washambuliaji hatari kabisa katika soka duniani.
Gazeti
namba moja la michezo Hispania la Marca, lilimpa tuzo ya usajili bora wa msimu
wa 2013-14 baada ya mafanikio makubwa ukiwa ni msimu wake wa kwanza Hispania.
Pia
akabeba Tuzo ya Mchezaji Bora wa Amerika Kusini kati ya wale wanaocheza La Liga
akiwapiga kumbo Angel Di Maria aliyeshika nafasi ya pili na Neymar aliyeshika
namba tatu.
Kama
ukipata nafasi mara nyingine, mfuatilie, huyu jamaa ni mbayaaa. Ana uwezo
mkubwa sana wa kufunga, si muoga wa mabeki wakatili kama Pepe au Sergio Ramos
na wengine wenye sifa hizo.
Amekuwa
na ndoto ya kuifunga kila timu bora kwa sababu anaamini kila mshambuliaji bora,
lazima aishinde safu bora ya ulinzi.
Bacca
ambaye alikuwa mchezaji bora wa mechi ya fainali ya Europa walipocheza na
Dnipro, juzi, ni mfano wa kuigwa, pia ni mchezaji ambaye Watanzania wanaweza
kujifunza mengi huenda kuliko kwa Messi na Ronaldo.
Mtu
huyu ni mchezaji aliyekubali kutimiza ndoto zake katika kipindi kigumu, kweli
ameweza na umri unakwenda lakini uwezo wake, haujawahi kuyumba.
0 COMMENTS:
Post a Comment