NINAAMINI
utakuwa umesikia malalamiko ya wagonjwa ambao wamekuwa wakilalama kwamba baadhi
ya wauguzi wa hospitali za serikali wamekuwa wakiuza dawa wodini.
Wauguzi
hao ambao ni watu muhimu sana katika taifa letu, wameamua kuwa wachuuzi wa dawa
kwa wagonjwa ambao baada ya kuandikiwa dawa, huambiwa hospitali haina dawa.
Baada
ya muda, wauguzi hao hupita wakiuza dawa na hapo ndiyo maswali yanaibuka.
Kwamba wanazitoa wapi wakati hospitali imesema imemaliza dawa. Swali au ndiyo
zile zilizotolewa na serikali, halafu zimefichwa na sasa wagonjwa wanauziwa?
Swali
jingine ni hivi, kama wauguzi ndiyo wanaouza dawa, unafikiri wanashindwa
kushirikiana na madaktari wawaandikie wagonjwa rundo la dawa ili wauguzi hao
wafanye biashara yao kwa faida kubwa?
Hakika
hali hii inaonyesha kiasi gani watu tunaopaswa kuwaamini wanavyopotoka na
kutuingiza hatarini na hofu kubwa ya maisha yetu hasa kwa wananchi wengi wa
Tanzania wasiokuwa na uwezo, si sahihi.
Wakati
tunaona wao wanafanya lisilo sahihi, najaribu kujiuliza maswali mengi kuhusiana
na viongozi wengi wa soka ambao kama ilivyo kwa wauguzi, wanavyoweka rehani uhai
wa soka la Tanzania ambalo hakika limekuwa likiendelea kupapasa huku wengi
wakitaka lisifiwe kuwa linapiga hatua.
Kila
mmoja anaweza kujisifia kwamba Tanzania inafanya vizuri kupitia klabu, mfano
Yanga au Azam zilizoshiriki michuano ya kimataifa. Jibu litakuwa ziliishia
palepale tulipozoea, kuwa “zilijitahidi”.
Nembo
yetu ni kujitahidi. Mwisho wa hilo utakuwa lini? Hakika ni lazima hadi watu
wakubali kubadilika kwenda katika njia iliyo sahihi na lazima viongozi wakubali
kuwa watu wenye fikra endelevu na wakubali kupambana kweli. Ukisema nichague
akili sahihi katika soka la Tanzania, basi nitachagua za mshambuliaji wa
Tanzania, Mbwana Samatta.
Miaka
mitano iliyopita, Samatta alikuwa tishio katika kikosi cha Mbagala Market
iliyokuwa inashiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania. Akacheza Simba nusu msimu
tu, lakini sasa ana mambo mengi sana naweza kumfananisha na wenyeviti wa klabu
kubwa za Yanga na Simba, matajiri wakubwa wa Tanzania.
Angalau
ukisema gari, Samatta anatumia Range Rover Vogue ambayo hata kama thamani
haitakuwa sawa na ile ya Yusuf Manji, Zacharia Hans Poppe na vigogo wengine wanaojulikana
katika soka, lakini hatuwezi kukwepa kuwa ile ni Range Rover.
Tena
ana vitu rundo, naweza kuonyesha anawazidi wachezaji wakongwe wenye majina
makubwa kwa zaidi ya miaka kumi sasa. Unawajua, fungua tu macho utawaona.
Umaarufu
wa Samatta kwa sasa unazidi ule wa mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden
Rage, wenyeviti waliopita wa Yanga kama Francis Kifukwe na wenzake, Mwenyekiti
wa zamani wa Fat, hata Rais wa sasa wa TFF, Jamal Malinzi.
Umaarufu
huo wa Samatta umepaa ndani ya miaka mitano, tena baada ya kucheza miezi
michache tu Ligi Kuu Bara ambayo wachezaji wengi wanaona ndiyo ndoto yao kuu.
Akaondoka
kwenda DR Congo kujiunga na TP Mazembe huku wengi wakiamini ni nadra, atakwama
na kurudi kama ambavyo wengine walivyoamua kurudi nyumbani akina Haruna Moshi
‘Boban’, Jerry Tegete, Shabani Kisiga na wengine wengi.
Kama
utani, kinda huyo amekwenda akapasua anga hadi sasa amekuwa mfano wa kuigwa
kila sehemu. Ndiyo maana nasisitiza kuwa nikiambiwa kuchagua, basi nitachagua
akili yake ambayo ndani imejaa ujasiri unaowashinda Watanzania wengi.
Ubinafsi,
kutaka kupata pekee, kutaka kushiba mwenyewe, kutamani kupaa kwa kujulikana
sana, ndiyo imekuwa sehemu ya tatizo kubwa ya maendeleo ya soka la Tanzania
ambalo kamwe siamini kuliita soka letu kutokana na udogo wake wa milele.
Sasa
inaonekana tunahitaji akili za Samatta kwa wauguzi ili wasiuze dawa wodini na
kuamini wanahitajika kuwasaidia Watanzania. Pia tunahitaji akili za kijana huyo
wa miaka 23, kuzipandikiza kwa viongozi wa klabu, vyama na hata shirikisho ili
mpira uende. Sijui hata kama zitatosha, aahh!
0 COMMENTS:
Post a Comment