Na Saleh Ally
KATI ya mwaka 1956 au 1957, Arsene Wenger
alikuwa kati ya vijana katika Kijiji cha Duttlenheim nchini Ufaransa waliokuwa
wakilazimika kulipa pauni 1 (Sh 2200) kwa ajili ya kuangalia mechi za Kombe la
FA.
Wenger ameeleza kwamba walikuwa wakilipa fedha
hizo na kupata nafasi kuangalia michuano hiyo huku wakishangazwa na namna mpira
ulivyokuwa ukiteleza vizuri katika nyasi.
“Zilikuwa ni nyasi ambazo hatukupata
kuziona, zilionekana na sura ya mvuto, ziliteleza vizuri na ilikuwa raha sana
kuona.
“Televisheni ya kijiji ya ‘black and white’
ilikuwa maarufu sana. Kwetu hakukuwa na televisheni hadi nilipofikisha miaka
15, wazazi wangu walifanikiwa kununua,” anasema Wenger.
Sasa
Wenger ni shujaa wa Kombe la FA, anakuwa kocha pekee katika karne hii
aliyefanikiwa kubeba kombe hilo mara sita.
Kombe kongwe na lenye heshima kubwa ndani ya
England, Wenger amefikisha mara sita na kumfikia George Ramsey ambaye
aliifundisha Aston Villa tangu mwaka 1884 hadi 1926.
Ndani ya miaka hiyo 42 ndiyo Ramsey
alifanikiwa kubeba Kombe la FA mara sita. Wenger amefanikiwa kubeba kombe hilo
mara sita ndani ya miaka 19, kumbuka alitua Arsenal mwaka 1996 akitokea Grampus
Eight ya Japan. Wakati huo Alex Ferguson alikuwa anatimiza mwaka wa 10 tangu
ajiunge na Manchester United aliyojiunga nayo akitokea Aberdeen ya Scotland.
Katika miaka hiyo 19, pia Wenger amebeba
ubingwa wa England mara tatu. Pia ameiwezesha Arsenal kukusanya Ngao za Jamii
mara tano.
Wenger sasa ameweka rekodi ya kuiongoza
Arsenal kufikisha makombe 12 ya FA ambayo ni mengi zaidi kwa klabu. Pia ndiye
kocha mgeni kutoka nje ya Uingereza kubeba makombe mengi zaidi.
Wakati akizungumza na waandishi wa habari,
aliwachekesha baada ya kusema hajui hata medali zake tano za nyuma zilipo,
lakini alikumbuka chache tu alipoeleza alizitoa katika shughuli za kusaidia
jamii, ziuzwe kama sehemu ya mchango wake.
Lakini aliwafurahisha aliposema kwamba,
nyingine huenda wale vijana ambao wamekuwa wakifanya usafi kwake, huenda ‘walizipitia’
na kusisitiza, yeye si mtu mzuri katika kazi ya kuhifadhi kumbukumbu.
Wenger ni kocha ambaye unaweza ukamzungumza
kwa njia zote na suala la ubora haliwezi kuwa mbali naye kwa kuwa amefanya
mengi ambayo inawezekana hata kocha mmoja hakuwahi kufanya katika dunia ya
mchezo wa soka.
Mfano
mzuri, alikuwa akichukua wachezaji walioonekana hawawezi tena, wamekwisha au ni
mizigo, halafu anaanza kuwasuka upya kabla ya kuibuka na kuwa tishio.
Mfano mzuri ni Thierry Henry ambaye alimtoa
Juventus ya Italia akionekana hakuwa na nafasi. Waitaliano hao walimnunua
kutoka AS Monaco, lakini kufika pale akakwama. Wenger akamtoa na kumuinua, wako
wengi.
Lakini inawezekana Wenger ndiye kocha
anayeongoza kwa kuwaamini wachezaji makinda ambao baadaye wanaibuka na kuwa
tegemeo wa Arsenal. Unawajua akina Nicholas Anelka, Cesc Fabregas na wengine
kibao kama Theo Walcott aliyemnunua akiwa kinda kutokea Southampton, kinda wa
miaka 17 akampa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza. Msimu ujao atakuwa lulu ya
dunia kwa kuwa baada ya kurejea ameonyesha tayari ni hatari.
Wenger pia anaweza kuwa kocha aliyebana matumizi
kuliko mwingine yeyote na bado akapata mafanikio ya juu zaidi. Arsenal ilikuwa
lazima ibane matumizi kutokana na madeni makubwa yakiwemo yale ya Uwanja wa
Emirates.
Pamoja na kubana matumizi hayo, Arsenal
imeendelea kuwa katika tano bora ya timu tajiri duniani. Imebaki katika nne
bora ya Ligi Kuu England na inapata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Huyu
babu afanye nini hasa? Makinda amewainua, faida ameingiza na hata makombe ya FA
anaongoza, Ligi Kuu England amechukua matatu. Awape nini Arsenal ili wamwamini
na kuona shujaa kwao?
Huenda hata Ferguson alionekana hana faida
sana wakati akiwa Manchester United. Kuondoka kwake, leo ni gumzo licha ya uwepo
wa kocha wa sasa. Inaonekana viatu vyake, kazi kubwa kuvalika.
Kwa
hali inavyokwenda, siku Mfaransa huyo mwenye miaka 56 akiamua kuondoka Arsenal,
wa kuvaa viatu vyake, ili aendane na mfumo wa Arsenal itakuwa kazi kubwa na
tatizo kwa Arsenal.
Huenda, huu ulikuwa wakati mzuri na mwafaka
kwa mashabiki wa Arsenal wakiwemo wale wa Dar es Salaam hadi Mwanza, Lindi hadi
Mara au Tanzania nzima na duniani kote pia kuonyesha kwamba kocha huyo naye ana
mchango mkubwa.
Hii
ni kwa kuwa, sifa nyingi za ubingwa wa FA kwa mara ya pili mfululizo kwa misimu
miwili iliyopita zinaonekana kwenda kwa waliofunga mabao.
Zinaonekana kwenda kwa mabeki na viungo
waliocheza vizuri, lakini si kwa Wenger na siku Arsenal ikiharibu, utasikia
mzigo wote anaangushiwa yeye. Kuna wakati najiuliza, labda Wenger ni Mnyamwezi?
0 COMMENTS:
Post a Comment