HIKI ndiyo kipindi cha neema kwa wachezaji
wanaotaka kuongeza mikataba mipya na timu zao katika Ligi Kuu Bara.
Mchezaji ambaye anakuwa amemaliza mkataba,
anataka kubaki katika klabu husika lazima atakuwa na nafasi ya kupata maslahi
zaidi.
Angalau kitu kidogo kutoka katika fedha ya
usajili, halafu fedha ya mshahara nayo inaweza kuongezwa pamoja na maslahi
mengine.
Kipindi cha usajili kinatakiwa kuwa cha
neema kwa wachezaji hasa wale ambao wamefanya kazi yao kwa kujituma kweli na
kuonyesha kuwa wao ni msaada na muhimu katika timu zao.
Kitakuwa cha furaha sana kwa waliofanya kazi
vizuri, wale waliokuwa wanategea, huenda kinakuwa kigumu kwa kuwa sauti yao
inakuwa chini. Hawawezi kupasa sauti kwa kuwa si wale wanaohitajika.
Hiki ndiyo kipindi cha usajili wa Ligi Kuu
Bara, kipindi ambacho kila klabu kulingana ana uwezo wake inajitahidi
kujiimarisha kulingana na mahitaji yake na uwezo wake kifedha.
Lakini utaona kuna migogoro kadha wa kadha
imeibuka, kuna watu wapya wa kila aina ambao wameibuka na kuwa wasemaji wa
wachezaji, mameneja au watu wanaozungumza kwa niaba ya wachezaji hao.
Hao wameibuka katika kipindi hiki, tena
inaonekana wamekuwa wakichangia pia kuwapotosha wachezaji hao kwa kuwa tu
wanalenga maslahi yao binafsi.
Mameneja hao, wamekuwa wakiwataka wachezaji
kutaja viwango vikubwa sana vya fedha vinavyosababisha hadi kukosa timu kwa
kuwa klabu zinaona kitita cha fedha kinachotajwa na uwezo wa mchezaji,
haviendani.
Tumeona wachezaji watatu au wanne waliokuwa
wasajiliwe na Yanga au Simba, walishindwa kutimiza ndoto zao kutokana na tatizo
hilo la dau kubwa kupindukia.
Dau linakuwa kubwa kwa kuwa wakala naye
anataka “cha juu”. Lazima amshawishi mchezaji kutaja dau kubwa ili naye apate
“maji ya kunywa”. Mwisho mchezaji anakosa timu ambayo angalau ingemlipa na
kumsaidia kupata nafasi ya kujitangaza zaidi.
Mchezaji anapotokea Mgambo au Stand United
na kujiunga na Yanga au Simba, hilo ni jambo moja la hatua kwa maana ya
kujitangaza zaidi iwe ndani au nje ya nchi. Anapoendelea kubaki katika timu
wakati ulikuwa wakati mwafaka wa kuondoka pia si sahihi.
Lakini ataendelea kubaki kwa kuwa wakala
alimlazimisha ataje Sh milioni 40. Wakati mchezaji alikuwa tayari kuondoka kwa
Sh milioni 20 na klabu ikamueleza itampa Sh milioni 25.
Kwa Sh milioni 25, maana yake klabu imeweka
nyongeza ya Sh milioni 5. Lazima mchezaji atakuwa tayari kwenda. Lakini meneja
anaona angalau apate fedha nyingi, hivyo anamshawishi aongeze zaidi huku akiwa
amesahau hana kiwango hicho kwa maana ya thamani.
Sikatazi wachezaji kuwa na meneja wao,
lakini nashauri wajipange na kuongozwa na watu wanaojua thamani ya mpira
kupitia mchezaji, nini maana ya usajili na ikiwezekana mipango kuanzia sasa na
baadaye.
Kusiwe na meneja wa haraka kwa maana ya kupata
fedha leo tu, hajali hata kama mchezaji atakosa timu. Wakati mwingine meneja au
wakala mwenye hesabu nzuri anaweza kuangalia mchezaji angalau apate nafasi
katika timu inayoweza kumsaidia kujitangaza, halafu maslahi makubwa yatafuata
baadaye.
Lundo la mameneja wasiojielewa au kujua hasa
kuhusiana na soka kunaweza kusababisha tatizo kubwa baadaye. Lazima kuwe na
wale ambao lengo la kutaka kumuendeleza zaidi mchezaji kwa ajili ya kumpa soko
kubwa zaidi.
Kama ikifikia kama ilivyo sasa, wakati wa
usajili, meneja ndiye anayetaka kufaidika zaidi hata kuliko mchezaji, basi hilo
litakuwa ni tatizo kubwa sana, hasa baadaye.
Wachezaji pia waangalie nani anayewasimamia,
lakini ikiwezekana, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), vizuri likatengeneza
utaratibu wa kuwatambua mameneja wa wachezaji kama familia ya mpira ili
wakifanya siku nyingine wapongezwe na wakiboronga, basi waadhibiwe.
0 COMMENTS:
Post a Comment