Mshambuliaji wa Yanga, Malimi Busungu sasa ameamua kufanya mazoezi ya ziada ili kukabiliana na ushindani mkubwa wa namba.
Busungu anayemudu kucheza namba tisa na 10, kwa sasa anapata
changamoto kubwa kutoka kwa washambuliaji wazoefu wa kimataifa wa timu hiyo,
Mrundi, Amissi Tambwe na Mzimbabwe, Donald Ngoma.
Kutokana na hali hiyo, Busungu ameamua kujifua vilivyo ili aweze
kuwa na uwezo mkubwa wa kucheza nafasi nyingi uwanjani kama ilivyo kwa kiungo
wa timu hiyo Salum Telela ambaye anaweza kucheza kwa ufanisi nafasi tano.
Busungu amesema kuwa anatamani zaidi kuwa miongoni mwa wachezaji
watakaokuwa wakiunda kikosi cha kwanza cha timu hiyo lakini kutokana na
ushindani wa namba uliopo katika kikosi hicho, imembidi afikie uamuzi huo.
“Huu ndiyo wakati wangu wa kupambana kwa sababu bado nina nguvu,
nikizembea nitashidwa kutimiza ndoto zangu.
“Ili niweze kupata nafasi katika kikosi cha kwanza, inabidi niwe
na uwezo mkubwa wa kucheza nafasi nyingi uwanjani na sasa najifua vilivyo ili
niweze kutimiza lengo langu hilo, nafanya mazoezi mara mbili kwa siku, asubuhi
nakuwa na timu na jioni nakuwa mwenyewe Coco Beach,” alisema Busungu ambaye
alisajiliwa na Yanga kwa kitita cha Sh milioni 25 akitokea Mgambo JKT ya Tanga.
“Nikiendekeza uvivu sitaweza kucheza kabisa mbele ya akina Tambwe,
Ngoma na Sherman ambao wamekuwa wakiniumiza kichwa kwelikweli.”
0 COMMENTS:
Post a Comment