MAVUGO... |
Beki wa zamani wa Simba, Mrundi, Said Kokoo, amewapambanisha kwa
kuwachambua kwa kina Warundi wenzake, straika wa Yanga, Amissi Tambwe na yule
wa Simba anayetarajiwa kutua hivi karibuni, Laudit Mavugo na kuweka wazi kuwa
Mavugo ni noma.
Mavugo na Tambwe wote ni raia wa Burundi, hivyo wanatarajiwa
kuonyeshana kazi kwa kushindana katika kuzisaidia timu zao kwenye mechi za ligi
kuu kwa kuwa wanajuana vizuri, huku pia uhasama wao ukichangiwa na kuwa kwenye
timu tofauti ambazo ni mahasimu wakuu hapa Bongo.
Beki huyo ambaye kwa sasa maskani yake ni hapa nchini, alisema
kuwa anawafahamu vizuri wachezaji wote hao kwani amekuwa nao karibu na kuwafuatilia
kwa kipindi kirefu mpaka hapa walipofikia, hivyo amebaini uzuri na ubora wa
kila mmoja.
Alisema kuwa sifa alizonazo Mavugo zinamfanya ampige ‘bao’ Tambwe
kwani aina yake ya uchezaji ambayo ni ya kasi inamruhusu kupiga chenga nyingi
za maudhi na kufunga kwa ufundi mkubwa lakini Tambwe vitu hivyo hana.
Aliongeza kuwa, japo Tambwe kuna vitu anamzidi Mavugo ikiwemo
uzoefu, kucheza kwa kujituma mwanzo mwisho pamoja na ujanja wa kukaa kwenye
nafasi nzuri za kufunga, lakini hivyo vinaweza kufanywa na Mavugo kadiri
atakapozidi kukomaa katika soka.
“Wote ni wachezaji wazuri japo wanatofautiana, Tambwe ni mzuri
katika kufunga lakini Mavugo ni mzuri zaidi kwani anafunga, ana spidi, chenga
nyingi, ndiyo maana Burundi alikuwa mfungaji bora mara mbili,” alisema Kokoo.
Mavugo ndiye mfungaji bora katika Ligi Kuu
ya Burundi baada ya kuzifumania nyavu mara 34.
“Tunamshukuru Mungu kwani muda wowote kuanzia
sasa, Mavugo atatua nchini kwa ajili ya kuungana na kikosi chetu baada ya
kufanikiwa kuvivuka vikwazo vyote vilivyokuwa vikikwamisha usajili wake,” chanzo
cha habari kiliwaambia waandishi wetu.
0 COMMENTS:
Post a Comment