Timu ya Simba imefanikisha usajili wa beki wa
pembeni raia wa Burundi, Emiry Nibomana kwa dau la dola 10,000 (zaidi ya
shilingi milioni 21).
Beki huyo mwenye uwezo wa kucheza namba 2 na 3,
tayari alikuwa visiwani Zanzibar ambako timu yake hiyo iliweka kambi kujiandaa
na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam, jana.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya
uongozi wa timu hiyo, beki huyo anayetoka nchi moja na straika wa Yanga, Amiss
Tambwe, amechukua kiasi hicho cha fedha akisaini mkataba wa miaka miwili ya
kukipiga Msimbazi.
Chanzo hicho kilisema wakati Nibomana akichukua
kiasi hicho kama dau la usajili, pia anatarajiwa kupokea dola 500 (sawa na
shilingi milioni 1) kama mshahara wake wa mwezi.
Kiliongeza kuwa Nibomana aliyetokea Vital’O
amesaini mkataba huo wa miaka miwili baada ya kufikia muafaka wa pande zote
mbili kati ya mchezaji na viongozi kabla ya kusaini mkataba huo.
Alipozungumza na gazeti hili, mchezaji huyo
alikiri kusaini mkataba na Simba kwa kusema: “Nimesaini mkataba wa miaka miwili
na nipo tayari kwa ajili ya kupamba na ushindani utakaokuwepo kwa kuwa mimi
mchezaji na hali kama hiyo ni ya kawaida.”
0 COMMENTS:
Post a Comment