Wakati mshambuliaji wa Yanga, Mzimbabwe, Donald Ngoma anatua
nchini akitokea kwao Zimbabwe baadhi ya mabeki wa Simba walimchukulia kama
mchezaji wa kawaida na kudai kuwa hatawasumbua siku watakapokutana naye
uwanjani.
Hata hivyo, juzi Jumamosi, mmoja wa mabeki hao wa Simba, Hassan
Isihaka ambaye aliwahi kusema kuwa watamdhibiti Ngoma, alishindwa kujizuia na
kujikuta akitamka kuwa mshambuliaji huyo wa Yanga ni hatari sana na ana roho
saba kama za paka.
Alisema katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam na kumalizika kwa Yanga kushinda mabao 2-0, Ngoma
ndiye mshambuliaji aliyewasumbua sana kuliko wengine wote na alikuwa hatari
sana kwao.
“Tulijitahidi sana kupambana naye na kumpatia vitisho vingi lakini
haikusaidia, jamaa alikuwa anakuja tu, hata haogopi.
“Ilifikia wakati tukaanza kumchezea faulo ili kumpunguza makali
lakini haikusaidia, aliendelea na kasi yake hiyo, hakika kwangu mimi huyo ndiye
mchezaji aliyetusumbua sana kuliko Amissi Tambwe na huyo Malimi Busungu,”
alisema Isihaka na kongeza kuwa jamaa inawezekana ana roho saba kama za paka
kwa sababu haogopi.
Hata hivyo, kwa upande wake Ngoma alipoulizwa kuhusiana na
upinzani alioupata kutoka kwa mabeki hao, alisema: “Soka siku zote hivyo ndivyo
lilivyo, ni mchezo wa kupambana.
“Nawapongeza mabeki hao wa Simba kwa mchezo wao waliokuwa
wakinichezea lakini namshukuru Mungu tumeweza kushinda, sijafunga mimi ila
wenzangu wameweza kufunga.
“Napenda kuwaambia Wanayanga kuwa nimekuja kufanya kazi na
nitapambana kila mechi ili kuhakikisha tunashinda na sitaogopa chochote kile,”
alisema Ngoma.
Mechi hiyo juzi ilikuwa ni mechi ya kwanza kwa Ngoma kuitumikia
Yanga dhidi ya Simba tangu alipojiunga nayo kwa kitita cha dola 50,000 akitokea
FC Platinum ya Zimbabwe. Mpaka sasa ameshaifungia timu yake hiyo mabao matatu
msimu huu wa ligi kuu.
0 COMMENTS:
Post a Comment