Na Saleh Ally
MECHI ya watani imepita, yaliyobaki lundo ambayo yametokea juzi
yanakwenda kuandikwa kwenye historia, tutayatumia kama kumbukumbu katika mechi
ijayo.
Yanga imeshinda kwa mabao 2-0 na kuondoa uteja wa kushinda mechi mbili
tu katika kumi zilizopita. Sasa itaingia uwanjani katika mechi ya mzunguko wa
pili ikiwa inajiamini.
Huenda Yanga watajiamini zaidi kwa kuwa hakuna dalili za Nani Mtani
Jembe hapa katikati. Maana yake, hadi pale watani watakapokutana katika Ligi
Kuu Bara, mzunguko wa pili.
Pamoja na Wanayanga wengi kufurahia kufuta ‘uonevu’ wa Simba,
mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe ni kati ya watu ambao wamekuwa na furaha
kuu ambayo haina kifani.
Tambwe alifunga bao la kwanza, halafu akasababisha bao la pili na
kumfanya aingie kwenye rekodi tamu kabisa ya Ligi Kuu Bara.
Rekodi hiyo inasema hivi, katika msimu wa 2015-16, Tambwe ameichezea
Yanga mechi nne, amefunga mabao manne, ametoa pasi nne za mabao.
Katika Gazeti la Championi, juzi Jumamosi, sehemu ya uchambuzi wa
mechi hiyo, katika makala yenye kichwa cha habari: “Maswali 7 ya kujiuliza”,
ilimuelezea Tambwe kama mshambuliaji hatari zaidi kuliko wengine kwa misimu
iliyopita.
Kwamba msimu wa 2013-14, Tambwe alikuwa mfungaji bora kwa kutupia
mabao 19 ‘kambani’. Msimu wa 2014-15 akitokea Simba kwenda Yanga, akamaliza
msimu akiwa na mabao 14, katika nafasi ya pili ya ufungaji bora nyumba ya Msuva
aliyefunga 17.
Sehemu ya makala hayo, ikasema hivi, ukimzuia Tambwe ndani ya dakika
90, lazima ujipongeze. Halafu ikahoji, Simba wamejipangaje?
Inaonekana walijipanga kweli, lakini kumdhibiti ikashindikana naye
akafunga bao na kutoa pasi ya kichwa cha kuparaza na Malimi Busungu akafunga
bao la pili mabeki wa Simba wakiwa wamepigwa ganzi ya kuzubaa, hasa Hassan
Kessy.
Mara baada ya mechi hiyo, Championi Jumatatu likafanya juhudi za
kumpata Tambwe akiwa ametulia ili kujua mambo kadhaa baada ya ushindi huo ambao
huenda utakuwa na maana kubwa kwake kwa kuwa Simba wakati inamuacha, iliona
hakuwa akifaa licha ya kwamba msimu uliopita, alikuwa mfungaji bora!
Wachambuzi kadhaa, walishangazwa na hali hiyo ya Simba. Kwamba Tambwe
si mshambuliaji mzuri kwa kuwa anavizia tu! Mzigo akatupiwa Kocha Patrick Phiri
kwamba yeye ndiye alitaka aachwe, lakini Phiri raia wa Zambia naye akauvua na
kusema, kamwe hakuwahi kusema hilo na angesema angekuwa mtu wa ajabu sana.
SALEHJEMBE: Ninaamini utakuwa na furaha sana kutokana na kufunga dhidi
ya Simba!
TAMBWE: Kweli nimefurahi sana, kwangu ilikuwa nzuri kwa kuwa nimeweza
kutimiza ndoto yangu.
SALEHJEMBE: Ndoto ipi tena?
TAMBWE: Nafikiri nimezifunga karibu timu zote nikiwa Simba pia Yanga.
Kubwa kama Azam, Mtibwa Sugar. Hata Yanga wenyewe, ilibaki Simba tu ambao
nilikuwa nikitaka sana kuwafunga.
SALEHJEMBE: Ilikuwa ni ndoto tu au ulitaka kufanya hivyo kuwaonyesha
kwamba walikosea kukuacha?
TAMBWE: Nilichokuwa nimelenga zaidi ni kuisaidia Yanga kupata ushindi
maana ndiyo timu ninayoichezea sasa na kuisaidia ishinde dhidi ya timu yoyote
ni jukumu langu.
SALEHJEMBE: Sasa kwa nini uonyeshe furaha kupindukia unapofunga dhidi
ya Simba?
TAMBWE: Furaha inatofautiana, kwanza nilikuwa sijaifunga Simba, lakini
si vibaya nikisema kudhihirisha kwamba naiweza kazi hii si kama ilivyosemwa
hapo awali. Pia kuonyesha Yanga hawakufanya kosa kuwa na mimi.
SALEHJEMBE: Kabla ya kufunga, ulifanya kitendo kimoja, ulidanganya kama
unapiga, ukausogeza mpira halafu ukapiga. Ulipanga au ilitokea tu?
TAMBWE: (Kicheko), awali kweli nilitaka kupiga, akili ya haraka
nikajua lazima mabeki wa Simba kwa kuwa ni wengi, wangeweka miguu au mwili.
Nikausogeza na kufunga. Nimeliangalia bao ni akili ya haraka sana, jambo ambalo
linanifanya nifurahi zaidi kama nafunga halafu linakuwa bao bora.
SALEHJEMBE: Hukuonekana kama una madhara katika mipira ya vichwa kama
ilivyozoeleka.
Tambwe: Inawezekana Simba walilifanyia kazi, walikaba sana pia
haikutokea nafasi nzuri sana.
SALEHJEMBE: Baada ya kufunga bao, ukaanza kuonyesha saa, nini hasa
maana yake?
TAMBWE: Simba walipofunga mabao matatu, aliyofunga Kiiza niliona
wachezaji wa Simba wakionyesha muda. Niliposoma mitandaoni walieleza kwamba
wanasubiri muda tu, tena wanaona unachelewa wanataka kutumaliza.
Sasa kwa kuwa tulianza kuwamaliza, ndiyo nilikuwa ninawakumbusha ule
muda umefika na sisi ndiyo tunawamaliza sasa.
SALEHJEMBE: Hukusikia uchungu kuifunga Simba ambayo mashabiki wake
walikuwa wakikuunga mkono sana hata baada ya uongozi kukutupia virago?
TAMBWE: Siwezi kusikia uchungu, ninafurahi kwa kuwa mimi ninafanya
kazi Yanga. Ila siwadharau mashabiki wa Simba na heshima kuwa ni timu yangu ya
kwanza kuichezea baada ya kuja Tanzania inabaki vilevile.
SALEHJEMBE: ‘Rafiki’ yako Hans Poppe atakuwa na huzuni, labda una
maneno yoyote ya kumueleza?
SALEHJEMBE: Fafanua kidogo hapo, vitendo kivipi?
TAMBWE: Mimi nitakuwa ninapambana kama mwanasoka, kazi yangu ni kucheza,
kufanya vizuri na kuisaidia timu yangu. Maneno nitamuachia yeye.
SALEHJEMBE: Kwa kikosi hicho cha Yanga na ushindi mara nne mfululizo,
kuna timu ya kuwazuia kweli?
TAMBWE: Ligi ni ngumu sana, mechi zinapishana na ushindi dhidi ya
Simba hauwezi kuwa jibu kwamba tutashinda mechi zote zijazo. Lazima tujipange.
SALEHJEMBE: Kila la kheri katika mechi nyingine za ligi.
Tambwe: Nanyi nashukuru kwa ushirikiano wenu tokea nikiwa Simba.
0 COMMENTS:
Post a Comment