October 24, 2015



Na Saleh Ally
Umeona kikosi Stand United kinavyokwenda katika Ligi Kuu Bara? Kamwe hauwezi kusema ni mwendo wa kusuasua hadi sasa.


Hata kama itakuwa imeanza vibaya, badi iko katika nafasi nzuri ya kuendelea kufanya vizuri kutokana na mwendo wake.

Stand United hadi sasa iko katika nafasi ya nne baada ya kucheza mechi nane ikiwa na pointi 15 na inafuatiwa na Simba yenye pointi kama hizo lakini zinatofautiana kwa michezo, Simba ina saba.
Pamoja na yote, bado inaonekana Stand United ina nafasi kubwa ya kuendelea kufanya vizuri zaidi ya hapo.

Historia ya kikosi hicho cha mjini Shinyanga inajulikana, ilikuwa ni timu ya wafanyakazi wa stendi ya mjini humo kwa ajili ya kujifurahisha.
Taratibu imekwenda inakua hadi ilipopanda daraja na ilitegemea mioyo zaidi.

Nasema mioyo kwa kuwa haikuwa na mdhamini na wafanyakazi wa mabasi mbalimbali wakiwemo makonda, mawakala na hata madereva walijitolea fedha zao kutokana na mapenzi.

Maendeleo yalifanya waaminike na hata ikafikia baadhi ya matajiri kuanza kusaidia kwa nia ya kupata maendeleo.

Sasa Stand United ina mkataba mnono kuliko timu zote kutoka Acacia Gold Mine. Wachimpaji hao wa madini ya dhahabu wameona ni jambo zuri kusaidia timu kutoka Shinyanga.

Jambo zuri ambalo linasaidia kukuza michezo nchini. Sasa inakuwaje kuanze migogoro na taarifa za kuingia watu ambao hawakuwa na msaada wowote kabla.

Najua ndani ya klabu hiyo kwa sasa kuna migogoro lundo, michache imeanza kujitokeza na baadhi iko chinichini.
Wenye tamaa ya fedha wanaona huu ndiyo wakati wa kuingia na kuanza kufanya vurugu ambalo si jambo jema.

Wameona kuna sehemu ya kushibisha matumbo yao, kabla ya mkataba huo wa Acacia hakuna hata mmoja aliyejitokeza. Walikaa kando kwa kuwa hawakuona kama kuna faida ya kuingia ndani.

Tafadhari wawape nafasi Stand United waendelea kutafuta maendeleo ya kikosi chao ikiwezekana kipate hata nafasi ya kucheza michuano ya kimataifa.
Wenye tamaa ya fedha wanapaswa kukaa kando na kuachana kama na tabia hizo zisizokuwa na msaada hata kidogo.

Tamaa ya fedha haipaswi kuwa muongozo wa maisha. Waliojitolea wawe mashujaa wa timu hiyo na wapewe nafasi ya kuisaidia kwenda mbele kwa kuwa kama walifanikisha ikiwa haina kitu, bado wana nafasi ya kuisaidia sasa ikiwa na mkataba mzuri.


Stand United itakuwa kwa ajili ya wao walioianzisha, wanaoishabikia, Wanashinyanga na Watanzania wote wapenda soka lakini si walafi wachache wanaotaka kufaidika sasa kwa kuwa wameona mamilioni yameingia.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic