STEWART HALL (KULIA) AKIWA NA KOCHA MKUU WA YANGA, HANS VAN DER PLUIJM. |
Uongozi wa Klabu ya Yanga umedhamiria
kumuondoa nchini Kocha wa Azam FC, Stewart Hall, kwa kutaka Bodi ya Ligi
kuvunja mkataba wake wa kuifundisha Azam FC, iwapo hatathibitisha madai ya
rushwa aliyoyasema katika mechi waliyokutana Jumamosi.
Stewart Hall, raia wa Uingereza, alitoa
tuhuma hizo katika mchezo uliowakutanisha vinara hao wa ligi kuu kufuatia
penalti waliyopewa Yanga dakika za mwisho iliyotokana na kipa, Aishi Manula,
kugongana na kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva.
Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha,
amefunguka kwa kusema, Stewart anatakiwa athibitishe madai yake ya rushwa
iliyotolewa katika mchezo huo na kudai kuwa wanalifikisha suala hilo kwenye
Bodi ya Ligi na iwapo atashindwa kuthibitisha, basi kibali chake cha kufundisha
soka hapa nchini kiondolewe.
“Tunatarajia kuandika barua Bodi ya Ligi
kwa ajili ya kumshitaki Stewart ili aweze kuthibitisha madai yake kuhusu rushwa
aliyosema kwani hilo ni kosa kisheria na atueleze ni nani aliyeitoa na iwapo hatatoa
vielelezo, inabiti tuchukue hatua zaidi.
“Tunataka kibali chake cha kufundisha
soka hapa nchini kiondolewe, yeye ni kocha mgeni na anatakiwa aondoke hapa
nchini na huo ndiyo msimamo wetu kama Yanga, tunataka aachane na soka letu,
kwani atakuja kutuharibia.
“Tuhuma zilizotolewa si sahihi, wao
walikuja kwa ajili ya rafu na sisi tulikwenda kwa ajili ya ushindi, kuna
wachezaji wetu watatu walitoka nje baada ya kuchezewa rafu lakini hakuna kadi
yoyote iliyotolewa, pia kipa wao Aishi Manula alimchezea rafu Msuva na
alitakiwa kupewa kadi nyekundu lakini hakupewa na imetolewa penalti
analalamika.
“Stewart anatakiwa awe na busara, timu
yake ya Azam inafanya mambo mengi ambayo siyo mazuri katika soka letu na
akiendelea na hali hiyo, tutayasema yote yanayofanywa na viongozi wa timu yake.
“Anatakiwa kuheshimu makocha wazawa na
soka letu kwa ujumla, kwanza ni mtu mwenye bahati kuendelea kufundisha Bongo
kwa kuwa hakuna kitu chochote kipya alichokifanya hapa nchini.
“Tunashangaa Stewart alipewa kadi ya kutokaa
kwenye benchi katika mchezo wetu lakini ameingia kwenye ‘Conference Room’
kuzungumza na waandishi pamoja na kutukana, licha ya kujua kuwa ni kosa na TFF
wamekaa kimya,” alisema Tiboroha.
Hata hivyo, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya
Ligi, Boniface Wambura, amesema bodi hiyo itakaa na kuchunguza tukio hilo kwani
kiutaratibu alitakiwa kupeleka malalamiko yake kwenye bodi hiyo.
“Kwanza hakutakiwa kuongea tu kwani kwa
sasa kuna utaratibu wa kupokea malalamiko na kuyafanyia kazi, Kamati ya Masaa
72, itakaa kupitia mechi nzima na pia tunaweza kumuita ili atoe ushahidi kwani
tuhuma za rushwa siyo kitu kidogo, unatakiwa uwe na ushahidi kamili,” alisema
Wambura.
0 COMMENTS:
Post a Comment