Kiungo Mganda wa Azam FC, Brian
Majwega ameliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kumpa ruhusa ya kuitumikia
klabu ya Simba ili kulinda kipaji chake.
Kiungo huyo raia wa Uganda alipeleka
barua TFF akiilalamikia Azam kwa kushindwa kumlipa mshahara kwa miezi sita
lakini anashangaa sasa inamwekea kauzibe ili asijiunge na Simba.
Mganda huyo mwenye uwezo wa juu wa
kupiga mipira iliyokufa amekuwa akifanya mazoezi na Simba kwa siku kadhaa hali
iliyozua mtafaruku mkubwa kati ya Simba na Azam.
Majwega ambaye anadaiwa kusajiliwa na
Simba kwa dau la Sh milioni 40, lakini bado kuna figisufigisu kwani Azam ambayo
ilimpeleka kwa mkopo KCCA ya Uganda kudai bado ni mchezaji wake.
Majwega alisema kuwa ni vyema, TFF ikaliwekea uzito suala lake hilo kwa
kulisikiliza kwa haraka kabla ya dirisha la usajili kufungwa ili kuondokana na
tatizo alilonalo.
“Lengo langu ni kucheza soka na
nimejipanga kuhakikisha nakuwa mchezaji mzuri na kuleta ushindani katika timu
yangu na hata katika timu tutakazokutana nazo.
“Nawaomba TFF kuhakikisha wanalisikiliza
suala langu kwa haraka zaidi ili niweze kuwa huru na kujiunga na timu
nyingine,” alisema Majwega.
Aidha, kwa upande wa Katibu Mkuu wa Azam,
Idrissa Nassoro, alipoulizwa juu ya mchezaji huyo, alisema Majwega bado ni
mchezaji wao kwa kuwa aliondoka huku akiwa bado na mkataba.
Kiungo huyo alisaini mkataba wa miaka
miwili na Azam na unatarajiwa kumalizika mwakani.
0 COMMENTS:
Post a Comment