Na Saleh Ally, Johannesburg
KIKOSI cha timu ya taifa ya soka ya Tanzania,
Taifa Stars, kimeweka kambi jijini Johannesburg, Afrika Kusini kujiandaa
na mechi dhidi ya Algeria.
Stars itaivaa Algeria katika mechi ya kuwania
kucheza Kombe la Dunia mwaka 2018. Mechi hiyo itapigwa Novemba 14 jijini Dar es
Salaam, kabla ya kurudiana Novemba 17 jijini Algiers.
Katika kambi ya Stars mjini hapa, karibu kila
kitu kimekuwa kikionekana kwenda vizuri na matumaini ni makubwa kuwa Stars
itafanya vizuri licha ya ubora wa Algeria.
Bado inaonekana kuna mgawanyiko kati ya
wapenda soka wengi. Wapo wanaoamini Algeria hawawezekani, lakini wapo wanaoamini
kujituma, kufanya kazi ya ziada, inawezekana kabisa Stars ikawashangaza wengi.
Katika mahojiano
na kocha wa Taifa Stars mzawa, Charles Boniface Mkwasa kuhusiana na hali ya
kambi yake na muendelezo wa mipango.
Kambi hiyo iliyo katika Hoteli ya Holiday Inn
Express ipo katika ulinzi mkali na utulivu wa hali ya juu.
Pia kambi hiyo imeandaliwa mpishi maalum ili
kuhakikisha chakula cha wachezaji kinakuwa salama na wanakula wanachokihitaji.
SALEHJEMBE: Tuanze moja kwa moja,
unaizungumziaje hii kambi ya jijini Johannesburg?
Mkwasa: Kwa ujumla kambi iko vizuri, iko
katika sehemu nzuri na salama. Tunaamini malengo ambayo tulikuwa tumeweka basi
tutayafikia.
SALEHJEMBE:Mazoezi ambayo umekuwa
ukifanya yanaonekana ni makali sana. Unaweza ukazungumzia kwa maana ya
kufafanua, hii maana yake nini?
Mkwasa: Wachezaji wametokea katika timu
tofauti, tumeanza kutafuta ‘fitnesi’ ya pamoja. Mazoezi ni magumu sana lakini
vijana wanaonyesha kujituma na huu ndiyo wakati mwafaka kufanya hivyo, kadiri
siku za mechi zinavyosogea, hauwezi kufanya hivyo.
SALEHJEMBE: Lakini wachezaji hao wanatokea
katika klabu zao walipokuwa wanacheza ligi. Kuna haja ya kuwafua kwa nguvu
hivyo?
Mkwasa: Ni kweli wametokea kwenye ligi, lakini
tumekuwa tukiwafuatilia kwa karibu na kuona fitnesi yao inapishana, ndiyo maana
tumeamua kutafuta ya pamoja.
SALEHJEMBE: Algeria ina wachezaji wenye
maumbo makubwa, warefu na wanatumia sana mipira ya juu. Mmejiandaa vipi
kupambana na hilo?
Mkwasa: Mpira kawaida una mipango yake, bahati
mbaya wachezaji wetu wengi wana maumbo madogo. Lakini hauchezwi kwa urefu.
Utaona kuna timu zina wachezaji wafupi, mfano wa Lionel Messi lakini bado zimefanikiwa.
Kumbuka Hispania, Brazil walikuwa wana
wachezaji wengi wafupi na wakabeba Kombe la Dunia.
Kikubwa tutajipanga kudhibiti mapema ujio wa
mipira ya juu. Vizuri tahadhari kabla ya hatari.
SALEHJEMBE:Taifa Stars inaanzia nyumbani,
mmejipanga vipi?
Mkwasa: Hakika mpira wa sasa hauna
nyumbani na ugenini. Lakini tumejipanga, tunajua tunatakiwa kuwa na matokeo
mazuri yatakayotulinda mechi ya ugenini.
SALEHJEMBE: Mechi dhidi ya Nigeria, pia
Malawi kikosi chako kilionekana kina makosa ya umaliziaji. Hili limefanyiwa
kazi kweli?
Mkwasa: Kuna matatizo hauwezi kuyamaliza kwa
siku mbili tatu. Tunaendelea kutengeneza kila mara tunapokuwa kambini ingawa
umakini ungeweza kujengwa zaidi katika klabu zao kwa kuwa sisi tunakaa na
wachezaji kwa muda mfupi sana.
Lakini hatuchoki, tunalifanyia kazi kila mara (suala
la umaliziaji) kuhakikisha mambo yanakwenda sahihi. Tunaendelea kulikemea, ila
halitaisha kwa siku moja tu.
SALEHJEMBE: Kuna mashabiki hadi sasa wanaamini
Tanzania kuifunga Algeria, au kuing’oa ni ndoto. Hili linakuvunja moyo?
Mkwasa: Mpira umebadilika sana, haujali
nyumbani au ugenini na wala hauendeshwi tena kwa historia. Tunawaheshimu sana
Algeria kutokana na ubora wao. Lakini tunataka kucheza nao na kushinda.
SALEHJEMBE: Ndiyo timu bora kabisa kutoka
Afrika. Hauoni ni timu hatari kwa kikosi chako?
Mkwasa: Kweli ni wazuri na bora, tunaheshimu
uwezo wao lakini tunachotaka ni kufanya vema na kushinda na katika mpira
kutokana na mabadiliko, inawezekana. Angalia Iceland imeifunga Uholanzi, kwa
sasa mambo hayo ni ya kawaida.
Utaona mechi na Algeria, wako walioamini
tutafungwa tatu au nne. Lakini tukaonekana ndiyo tulistahili kushinda, lakini
hatukuwa makini.
SALEHJEMBE: Hamkuwa makini, unafikiri mechi
ijayo umakini umeongezeka?
Mkwasa: Kadiri tunavyojifunza,
inawezekana kabisa. Wachezaji wasikilize na kuelewa mafunzo yetu, halafu
wayafanyie kazi. Ninaamini itawezekana.
SALEHJEMBE:Ikitokea umewakosa Thomas
Ulimwengu na Mbwana Samatta. Unaamini kikosi ulichonacho hapa Johannesburg,
kinaweza kupambana na Algeria na kushinda?
Mkwasa: Siwezi kufananisha ujuzi wa kila mmoja
binafsi, pia siombi wasiumie. Lakini katika mpira lolote linawezekana.
Tumewachagua vijana tuko nao hapa, ni bora na wanaweza kucheza ingawa watakosa
uzoefu ambao wanao kina Samatta na Ulimwengu na kweli tunauhitaji sana uzoefu
wao. Kwa vijana kupangwa dhidi ya timu kama Algeria, si kitu kidogo. Wazoefu
kama Ngassa na wengine wapo, lakini ninaamini tutapambana.
SALEHJEMBE:Mwisho kwa Watanzania wapenda soka,
una lolote la kuwaeleza?
Mkwasa: Sisi tuko hapa tunapambana sana,
natamani wangeona kila jambo. Nia yetu ni kupigania taifa la Watanzania, nao
wakiwa ndani. Hivyo siku hiyo waje, vijana wakiona watu wanawaunga mkono nao
wataongeza juhudi zaidi, watajua wana deni. Nawakumbusha sisi tunafanya kazi
kwa niaba yao Watanzania. Waje kwa wingi tuungane kupambana na Waalgeria ambao
watakuwa wakitusubiri kwao kuungana na mashabiki wao ili watuchanganye.
0 COMMENTS:
Post a Comment