November 6, 2015


Siku takribani saba baada ya kutokea kwa vurugu za mashabiki wa Coastal kutaka kuwashambulia waamuzi waliochezesha mchezo wa timu hiyo dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga, makubwa yameibuka juu ya kilichotokea nyuma ya pazia.

Katika vurugu hizo, baadhi ya mashabiki wa Coastal walilalamikia maamuzi kadhaa ya mwamuzi wa mchezo huo, ikiwemo kuwapa penalti Mbeya City dakika za mwishoni mwa mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliomalizika kwa sara ya bao 1-1, hivyo kusababisha amani kutoweka lakini askari polisi waliwahi kuingilia na kuchukua hatua.
Taarifa ambazo gazeti hili limezipata ni kuwa kwa kuwa vurugu hizo zilitokea wakati waamuzi wakiwa uwanjani hawajaingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, kuna mashabiki waliovamia vyumba hivyo na kuvunja kisha kuingia ndani na kuiba mali za waamuzi hao waliochezesha mchezo huo.
Baadhi ya mali zilizoibiwa ni simu, nguo za michezo na fedha.
Mmoja wa viongozi anayeishi karibu na Uwanja wa Mkwakwani amesema:
“Ndiyo waamuzi waliibiwa vitu vyao, uharibifu ulikuwa mkubwa, achana na ule wa kuvunja vifaa vya waamuzi wa akiba kama ilivyoonekana kwenye runinga,” alisema kiongozi huyo na kuongeza:
“Unajua kuna vitu vinaendelea vingi nyuma ya pazia, naamini hata hiyo ripoti ya mwamuzi wa mchezo huo, sidhani kama itaeleza uhalisia wa vurugu zilizotokea na kuwa mchezo huo ulivunjika.

“Ndiyo mchezo ulivunjika kwa kuwa mwamuzi hakupata muda wa kumaliza mchezo kwani tayari alikuwa amevamiwa, kuna ushawishi mkubwa kutoka kwa***(anamtaja jina, ni kiongozi wa juu wa soka) ndiyo maana hata maamuzi yatakayochukuliwa sidhani kama yataendana na kosa lenyewe.
 “We si unaona, lile sakata la (Juma) Nyosso lilichukuliwa kwa uzito wakati hili ambalo lilikuwa likitishia maisha kabisa ya watu linapotezewa.
“Kila mwanasoka anajua adhabu ya timu inayohusika kuvunja mchezo, licha ya kuwa mpira ulikuwa ukielekea mwishoni, lakini mwamuzi hakuumaliza mchezo huo.”
Alipoulizwa Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura kuhusiana na vurugu hizo alisema: “Tumeipata ripoti lakini kwa kuwa ni suala la kinidhamu tumepeleka suala hilo kwa Kamati ya Nidhamu, waulizeni TFF au kamati husika juu ya nini kinachoendelea.”

Alipoulizwa Katibu Kuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa, alisema: “Hiyo barua haijafika mezani kwangu, kwa hiyo siwezi kulizungumzia.”

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic