January 12, 2016



Muda wa Kocha Dylan Kerr kuinoa Simba umefikia mwisho baada ya uongozi kwa pamoja kukubaliana kuachana naye rasmi.

Uongozi wa Simba umefikia uamuzi wa kuachana na Kerr baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa kikosi hicho katika Ligi Kuu Bara na baadaye Kombe la Mapinduzi lililomalizika hivi karibuni mjini Zanzibar.
Pamoja na kutokuwa na matokeo mazuri lakini inaonekana uongozi haujaridhishwa na uchezaji wa kikosi cha timu hiyo na mambo yalikuwa mabaya zaidi katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar.

“Kweli kamati ya utendaji imefanya kikao cha muda cha dharura na kukubaliana na hilo,” kilieleza chanzo kutoka Zanzibar.

“Taarifa tulizonazo ni kwamba kocha Kerr ameitwa Dar es Salaam ambako ataondoka kesho Jumanne akiwa Dar es Salaam ataelezwa kuhusiana na uamuzi huo wa uongozi kumtupia virago na nafasi yake atapewa Kocha Majanja ambaye juzi aliingia mkataba kama kocha msaidizi.”

Chanzo kilipoulizwa kama uongozi hauwezi kubadili uamuzi hiyo kesho, kilieleza:

"Tunaamini hakuna nafasi hiyo, hata Kerr mwenyewe ameishashitukia, atakuwa anajua kwamba mambo yatakuwa hivyo. Usiku huu ameamua kutoka kwenda kuiaga Zanzibar (kicheko)."

Taarifa nyingine zimeeleza kwamba Kerr raia wa Uingereza ameponzwa na ubishi na uongozi umekuwa ukimlaumu kutofanya kazi kwa kujituma.

Wakati fulani, Rais wa Simba, Evans Aveva aliwahi kujitokeza mazoezini kimyakimya wakati Simba ikijifua kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), hali iliyoonyesha wazi uongozi hauridhiki na utendaji wa Mwingereza huyo aliyechukua nafasi ya Goran Kopunovic aliyeondoka baada ya kutaka dau la Sh milioni 100 ili aongeze mkataba mpya Simba.

Kerr anaondoka na kuiacha Simba katika nafasi ya tatu baada ya mechi 13 na imekusanya pointi 27 nyuma ya Yanga yenye 33 na Azam FC kileleni ikiwa na 35.

Mwingereza huyo anaiacha Simba ikiwa imeshinda mechi 8, sare 3 na kupoteza mbili, imefunga mabao 20 ikishika nafasi ya tatu kwa ufungaji baada ya Yanga yenye 30 na Azam FC yenye 27 huku ikiwa imeruhusu mabao 9, ikiwa safu bora ya ulinzi katika nafasi ya nne baada ya Azam iliyoruhusu mabao 8, Mtibwa Sugar mabao 7 na Yanga yenye safu ngumu zaidi imefungwa mabao matano tu.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic