Straika mkongwe wa Simba, Mussa Mgosi, leo anatarajiwa kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha Kocha Jackson Mayanja akichukua nafasi ya Ibrahim Ajib.
Ajib ameondolewa kwenye kikosi hicho baada ya kupata majeraha ya mgongo kwenye mechi dhidi ya Mtibwa Sugar iliyochezwa wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mkongwe huyo ambaye hadi sasa hajafanikiwa kufunga bao, amekuwa hana nafasi kikosi cha kwanza lakini leo Jumatano ana nafasi ya kucheza kwenye kikosi hicho kitakachoivaa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa.
Katika mazoezi ya juzi, Mayanja alionekana akimpa baadhi ya maelekezo Mgosi wakati mazoezi hayo yanaendelea kwenye Uwanja wa Boko Beach Veteran Dar.
Mayanja akiendelea na mazoezi hayo, alipanga vikosi viwili kati ya hivyo kimoja alikipanga kile kitakachoanza kwenye mechi ya leo dhidi ya JKT Ruvu.
Katika kikosi hicho, Mgosi alipangwa kuanza kucheza namba 10 iliyokuwa inachezwa na Ajib huku Mganda, Hamis Kiiza akicheza namba tisa.
Wakati mazoezi hayo yanaendelea, washambuliaji hao walionekana wakicheza kwa kuelewana ndani ya uwanja ikiwemo kutengenezeana pasi za kufunga mabao.
Akizungumza mara baada ya mazoezi hayo Mayanja alisema katika kikosi chake anampanga mchezaji kutokana na kiwango anachokionyesha.
“Mchezaji atakayenionyesha kitu mazoezini ndiye atakayecheza na siyo kitu kingine chochote, ninafurahia kuona mabadiliko makubwa ya wachezaji wangu tangu nimefika,” alisema Mayanja.
0 COMMENTS:
Post a Comment