Na Saleh Ally
GUMZO kubwa kwa wiki yote imekuwa ni ile ishu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na ndugu zao Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) kuamua kuiruhusu Azam FC kwenda kushiriki bonanza nchini Zambia na kuachana na Ligi Kuu Bara.
Uamuzi huo wa TFF na TPLB unaonekana kuwachanganya watu wengi kwa kuwa ni kitu kinachoshangaza na si rahisi kufanywa na watu walio makini.
Huenda ingekuwa ni ugomvi kusema TFF si watu makini, lakini kitendo cha Rais wa TFF, Jamal Malinzi kukubali kwamba walichokifanya si sahihi, tayari uthibitisho wa hilo, uko wazi, kwamba hawakuwa makini.
Nilieleza jana katika makala niliyoandika kuhusiana na suala hilo, kwamba Malinzi aliyesema yote hayo yaliamuliwa wakati akiwa nje ya nchi, anaponzwa na kuchagua watu wenye uwezo mdogo katika nafasi nyeti ambazo zinahitaji msukumo kuliweka gurudumu vizuri kwenda na kasi sahihi.
Kujaza watendaji kwa kigezo cha ushikaji au “ahsanteni sana” ni tatizo kubwa na hili ndilo linaloitafuna TFF, ninaamini kama Malinzi angekuwa muungwana, basi kuomba radhi kwa juzi kungekuwa ni mara ya 300.
Ila wakati hiyo juzi akiomba radhi, kuna jambo alilisema kwamba Azam FC watakaporejea watakuwa kwenye mateso kwa kuwa watacheza ligi mara mbili kwa wiki na utakuwa mzigo kwao.
Wakati akisema hayo, waandishi wakamsikiliza na kuripoti, Malinzi alijisahau kwamba alikuwa akitangaza adhabu kwa klabu nyingine ambazo zinahusika kwa kuwa Azam FC kamwe haiwezi kucheza pekee, lazima kuwe na mpinzani.
Sasa ushiriki wa Azam FC kwenye hilo bonanza la Zambia, utawaumiza wengine kwa mujibu wa maneno ya Malinzi ambaye amesema anataka Azam FC ilingane michezo na wengine ili kuondoa hisia za masuala kama kuna timu inapendelewa au inapewa nafasi ya kufanya ujanja.
Kama Azam FC itacheza mechi mara mbili kwa wiki, basi timu zitakazocheza nayo ile mechi ya pili kwa wiki, pia zitalazimika kuingia ndani ya adhabu hiyo ambayo wao hawakuwa wahusika na haiwahusu kabisa.
Mfano Azam FC ilitakiwa kucheza mechi yake dhidi ya Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, leo. Haitakuwepo na Prisons watakuwa wanazubaa tu hadi hapo watakapopangiwa mechi mfululizo ili wacheze na Azam FC pia waendelee na ratiba ya kawaida, adhabu hii inatokana na nini?
Malinzi anaamini Azam FC kucheza mechi mbili mfululizo kwa wiki ni kama adhabu. Lakini anasahau adhabu anayoitangaza sasa inawahusu Prisons, Stand United na Mwadui FC ambao walitakiwa kufuatia kucheza na Azam FC kama ingekuwa haijapata ruhusa ya kwenda kushiriki bonanza la Zambia ambalo kwa hali ya kawaida linaonekana kuwa na thamani ya juu kuliko hata ligi yetu.
Katika makala ya jana, nilikuwa nikisisitiza suala la kuendelea kumpigia gitaa Malinzi kwa kuwa TFF inaendeshwa bila ya kufuata kanuni, sheria au kwenda kishikaji na watu kuangalia matakwa au maslahi yao binafsi.
Mfano mzuri utaona hivi, si rahisi kusikia timu zilizotakiwa kucheza na Azam FC zikipewa taarifa mapema na kwa maandishi. Kama ikiwa hivyo labda wafanye hivyo baada ya kusoma hapa. Kabla nimezungumza na viongozi wa timu hizo, kamwe hawajui lolote zaidi ya mawasiliano ya simu baada ya kusikia kwamba Azam FC wanasafiri.
Sina shida na Azam FC ambao kama wangezuiwa, wasingekuwa na ubavu wa kuondoka, lakini kwenye hili nitaendelea kuwa mkweli, kwamba TFF inaendelea kugeuka tatizo kuu la mchezo wa soka badala ya kuwa mlezi, mzazi na mwendelezaji mwenye uchungu.
Niko palepale, TFF ina watu wengi wasiokuwa na uwezo sahihi kulingana na vitengo walivyopewa. Hivyo lazima kuwe na mabadiliko kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri na kuepukana na kufanya mambo kama hili la Azam FC ambalo linaweza kuchangia hata kuendelea kuichosha timu hiyo, ikashindwa kabisa kufanya vizuri katika michuano hiyo ya kimataifa ambayo itakuwa na faida na nchi, eti kisa, wamekwenda kwenye bonanza!
Januari 30, 2016
Prisons Vs Azam Sokoine (HAIPO)
Februari 3, 2016
Azam Vs Stand Azam Complex (HATIHATI)
Februari 7, 2016
Azam Vs Mwadui Azam Complex (TUTAKUAMBIA)
Februari 13, 2016
Coastal Vs Azam Mkwakwani (KAMA HAITAAHIRISHWA, IPO)







0 COMMENTS:
Post a Comment