TAMBWE |
Kile kipigo cha mabao 2-0 ambacho timu ya Yanga ilikipokea wikiendi iliyopita kutoka kwa Coastal Union ya jijini Tanga, bado kinaziumiza nafsi za wachezaji wa timu hiyo ambapo mshambuliaji Amissi Tambwe amesema uwanja ule ni mgumu kwao.
Yanga walipokea kichapo hicho cha kwanza kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga sehemu ambayo wamekuwa wakikutana na upinzani mkali mara kwa mara.
Mpaka sasa Yanga imemaliza mechi zake tatu za ligi kuu ilizokuwa ikitakiwa kucheza kwenye uwanja huo dhidi ya JKT Mgambo, African Sports na Coastal Union, lakini haitazisahau kutokana na upinzani mkubwa iliokumbana nao kutoka kwa timu hizo baada ya kuambulia pointi nne tu kati ya tisa.
Mbali na kichapo cha Coastal Yanga pia ilitoka suluhu na Mgambo kwenye uwanja huo, huku wakiwafunga African Sports bao 1-0 dakika za lala salama.
Tambwe mwenye mabao 13 kileleni alisema kuwa mechi zote za Yanga ambazo ilicheza katika uwanja huo hazikuwa nyepesi.
“Hakuna mchezaji aliyefurahia kipigo hicho lakini ndivyo hivyo tena, imeshatokea, tunapaswa kujipanga kwa ajili ya mechi zetu zijazo ikiwemo ile ya Jumatano (leo) dhidi ya Prisons.
“Hata hivyo, naweza kusema kuwa safari hii Uwanja wa Mkwakwani ulikuwa ni mgumu sana kwetu kwani hakuna mechi iliyokuwa nyepesi, tulicheza na Mgambo hali ilikuwa ni ngumu kwani tuliambulia pointi moja.
"Tukacheza na African Sports tukapata ushindi dakika za majeruhi na mwisho wa siku tukafungwa na Coastal Union, hivyo kwa hali hiyo hatupaswi kulaumiana bali tujipange kwa ajili ya michezo ijayo,” alisema kinara huyo wa mabao kwenye ligi.
0 COMMENTS:
Post a Comment