March 23, 2016Na Saleh Ally
NILIWAHI kuwa karibu kabisa na Kocha Charles Boniface Mkwasa wakati akimueleza beki Abdi Banda wa Simba, kwamba kama hatakuwa makini basi hatamwita katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars.

Mkwasa alikuwa akimpa maneno hayo Banda wakati Taifa Stars ikiwa kambini nchini Uturuki kujiandaa na Algeria katika mechi ya kupambana kucheza hatua ya makundi ili kuwania kucheza Kombe la Dunia.

Katika mazoezi makali ya siku mbili za mwanzo, Banda aliumia njama za paja. Kitaalamu Mkwasa akasema mtu ambaye anakuwa si fiti ndiyo rahisi kuumia. Pia akamkumbusha Banda hiyo ni mara ya pili anamwita, halafu anaumia akiwa kambini na tatizo ni hilohilo!

Maneno ya Mkwasa yalikuwa yanamanisha kwmaba Banda hakuwa akifanya mazoezi ya kutosha na hakuwa makini. Kweli utaona, hadi leo hajawahi kumwita.

Banda ni mchezaji mwenye kipaji tena cha kucheza nafasi zaidi ya mbili katika safu ya ulinzi. Anajiamini na anaweza kufika mbali akiwa makini. Lakini anavyokwenda inaonekana hataki kufika mbali au inawezekana atabadilika, “baadaye akiamua”.

Sasa mjadala ni yeye, ni baada ya kugoma kupasha mwili alipoambiwa na Kocha, Jackson Mayanja ambaye alitaka Banda apashe baada ya kuona Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, amekosea kupiga krosi kwa mara ya pili.


Banda badala ya kupasha, akahoji vipi Tshabalala atolewe wakati kakosea mara moja tu! Hivyo hakusimama kupasha na hapo ndipo saga linaanzia. Wapashaji wanasema dakika chache baadaye Tshabalala alitoa krosi safi ambayo ilitua kichwani mwa Danny Lyanga na kuandika bao la kwanza la Simba dhidi ya Coastal Union. Banda akahoji, kwamba “si unaona sasa?”

Ukisoma taarifa za kwenye mitandao, hakika ni uozo mtupu kwa kuwa watu wanahoji na kumuunga mkono kuwa Banda alikuwa sahihi, tena anaonyesha mapenzi kwa mwenzake Tshabalala.

Huwezi kusema Mayanga hajui ubora wa Tshabalala, asingeuona basi asingemchezesha. Pia suala la nani anaingia, nani haingii haliwezi kuamuliwa na Banda. 

Mwenye uamuzi wa mwisho ni Mayanja, kama atakosea basi mzigo utakuwa ni wake. Alichotakiwa kufanya Banda ni kusimama na kuacha kupasha mwili.


Kwani nani anasema ukipasha misuli lazima uingie? Hauwezi kujua huenda ilikuwa mbinu ya Mayanja kumuonyesha Tshabalala akifanya mzaha tena, ataingia Banda hivyo ajitume zaidi.

Simba itakuwa ni timu ya ajabu kabisa kama “wendawazimu” wakiendelea “uendawazimu” uendelee kufanyika ndani ya timu hiyo. Kama kocha atakuwa na uamuzi wa kupanga na wachezaji wakawa na uamuzi wa kupanga timu!

Mara ya mwisho, Mayanja alikuwa na mgogoro na Hassan Isihaka na wenyewe ulihusiana na jambo kama hilo. Mayanja anampanga Isihaka acheze katika mechi ya Kombe la FA dhidi ya Singida United, yeye akahoji kama likizo yake imeisha kwa kuwa hakupewa nafasi ya kucheza dhidi ya Yanga!

Leo Banda anaambiwa aingie, naye anahoji! Lakini bado kuna wale wanaoona ni sahihi kama ambavyo Hamisi Kiiza alivyotetea upuuzi alioufanya Isihaka. Lakini siku chache Isihaka akaonyesha uungwana na kuomba radhi, jambo ambalo lilimuacha Kiiza na aibu, akaanza kutupia lawama vyombo vya habari jambo ambalo lilikuwa ni uzushi mtupu.

Kiiza kutetea makosa ya kijinga ya Isihaka ilikuwa ni kushindwa kujitofautisha na wachezaji makinda kama Isihaka. Lakini kwa shabiki au mwanachama wa Simba, kutetea kosa hili la Banda ni kuzidi kummaliza kwa sababu za kijinga pia.

Siku Mayanja akikosea, ataelezwa bila ya kificho.  Lakini leo tuwalinde wadogo zetu kwa kuwaeleza ukweli kwamba wanachofanya si sahihi. Hatuwezi kujenga kizazi cha wakosefu na wasumbufu wa baadaye kwa ajili ya kujifurahisha leo. Vema tukatumia akili “nyingi” na kuachana na “kidogo” yenye faida leo na hasara kubwa kesho.


1 COMMENTS:

  1. Katika watu wasiojitambua nawe saleh ni mmoja wapo kwani kazi yako ni kulamba viatu vya waliojuu yako siku zote.Nyie si mlimpora Banda toka coastal union kwa kisingizio kuwa hakulipwa mshahara,mlitegemea afanye nini akiwa kwenu?Mshahara wa dhambi ni mauti na mwosha uoshwa sasa acheni kulalama.

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV