MSUVA |
Kiungo mwenye kasiwa Yanga, Simon Msuva, amefunguka kuwa ni ngumu kwao msimu huu kuweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kutokana na kuwa na michezo mingi ya mikoani tofauti na wapinzani wao wanaongoza ligi hiyo licha ya kuwa na michezo ya viporo mkononi.
Simba inaongoza ligi kwa pointi 57 ikiwa imecheza michezo 24 nyuma Yanga yenye pointi 50 na michezo 21 sawa na Azam FC inayokamata nafasi ya tatu ikiwa na pointi 50, hivyo kuweka pengo la tofauti ya pointi saba kitu kinachomuumiza kichwa nyota huyo ambaye msimu uliopita aliibuka kuwa mfungaji bora wa ligi baada ya kufanikiwa kufunga mabao 17.
Msuva amesema kuwa ni ngumu kwao kuanza kuzungumzia ubingwa kutokana na tofauti kubwa ya pointi walizoachwa na wapinzani wao licha ya kuwa na michezo mitatu mkononi ambayo bado hawajaicheza mpaka sasa kutokana na ushiriki wao katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Unajua ligi imekuwa ngumu na kila timu inahitaji matokeo ya ushindi kwa sababu zipo ambazo zinahitaji kuepuka kushuka daraja sasa lazima tupambane ili kuweza kupunguza pengo la pointi tulizoachwa na Simba ambao ndiyo wanaongoza kutokana na wao kucheza michezo mingi tofauti na sisi, hivyo inakuwa ngumu kusema ni rahisi kuweza kuchukua ubingwa.
“Lakini changamto inakuwa kubwa kwa sababu tuna michezo mingi ya mikoani ambayo mara nyingi inakuwa migumu kutokana na ubovu wa viwanja tofauti na tunacheza hapa Uwanja wa Taifa sasa lazima nguvu ya ziada itumike ili tuweze kutetea ubingwa wetu maana uwezo wa kushinda michezo iliyobakia bado tunao,” alisema Msuva.
0 COMMENTS:
Post a Comment