Wekundu wa Msimbazi, Simba kesho Jumapili inacheza na Azam FC mechi ya Ligi Kuu Bara, licha ya kuwa katika mazingira magumu lakini inaweza kutwaa ubingwa na kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.
Ili timu ipate nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika michuano hiyo ni lazima ama iwe bingwa wa ligi kuu ishiriki Ligi ya Mabingwa au ibebe Kombe la FA ili ishiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Simba imebakisha nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika tu, hivyo ni lazima itwae ubingwa wa ligi kuu. Katika ligi hiyo ipo nafasi ya tatu na pointi 57. Ya kwanza ni Yanga ina pointi 62 na ya pili ni Azam yenye pointi 58.
Timu zote zimebakisha mechi tano kwani zimecheza michezo 25 hadi sasa. Ili Simba itwae ubingwa inatakiwa ishinde angalau mechi zake zote huku ikiomba Yanga ipoteze mechi zake.
Kama ukibisha we bisha tu, lakini Simba imejipanga kushinda mechi zake zote zilizobaki za ligi kuu na huku ikiziombea Yanga na Azam zifungwe mechi zake hata nusu yake ili yenyewe itwae ubingwa.
Pia Simba imepata nguvu kwani Yanga inacheza ugenini mechi zake zote zilizobaki, hivyo kuwa na uwezekano wa kupoteza baadhi yake.
Tofauti na hapo hata kama Yanga ikiwa bingwa wa FA na ligi kuu, Azam itakayoshika nafasi ya pili FA ndiyo itakayocheza Kombe la Shirikisho.
Kocha wa Simba, Jackson Mayanja amewahi kuliambia Championi Jumamosi kuwa, mkakati wake ni kushinda mechi zote zilizobaki ili kuweka mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa.
“Lolote laweza kutokea hapo, nimewaweka sawa kisaikolojia wachezaji wangu ili tupate ushindi katika kila mechi na tunaomba wapinzani watetereke,” alisema Mayanja.
0 COMMENTS:
Post a Comment