May 21, 2016

DIDA AKIWASALIMIA MASHABIKI, JANA.
Kipa wa Yanga, Deo Munishi ‘Dida’ jana alipokelewa kwa kubebwa juu juu na mashabiki wa timu yake muda mfupi baada ya kuwasili nchini akitokea Angola na timu yake.
Yanga imewasili nchini baada ya kutinga hatua ya makundi (nane bora) ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola kwa jumla ya mabao 2-1.

Awali Yanga ilishinda mabao 2-0 nchini kabla ya kufungwa bao 1-0 ugenini Jumatano wiki hii.

Katika mchezo huo, Dida alipangua penalti ya Esperanca dakika ya 90 na kuiwezesha Yanga kufungwa bao 1-0 pekee na kufuzu makundi.

Akizungumza na baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jana mchana, Dida alisema: “Walituonea sana, roho zao mbaya zimewaponza.

“Pamoja na mimi kuonekana shujaa lakini hiyo imetokana na nguvu ya timu nzima kucheza kwa ushirikiano, maana nisingeweza peke yangu, hakika tulipambana kiume.”

Akiwa uwanjani hapo, Dida alijikuta akibebwa juu juu na umati wa mashabiki uliojitokeza kuilaki Yanga ikitokea Angola ambapo iliwasili kwa ndege ya South African Airways.


Mashabiki wengi walijitokeza kuwapokea mashujaa hao wakiwa na pikipiki na magari yao. Waliondoka uwanja wa ndege kwa msafara wa pikipiki na magari kiasi cha kusimamisha shughuli zote kuanzia Uwanja wa Ndege hadi Quality Plazza waliposimama kwa muda, wakati wote watu walikuwa wakiwashangilia njiani kwa furaha kuu.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV