May 21, 2016


Na Saleh Ally
Achana na ule ushabiki wa Yanga na Simba au ule wa Ali Kiba na Diamond, hapa zungumzia uzalendo au Utanzania.

Ali Kiba amesaini mkataba na kampuni ya Marekani ya Sony, mkataba ambao ni nadra kusikia msanii wa Tanzania amepata. Hili ni jambo la kujivunia kwa Watanzania.

Angalia Yanga, wameitinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho. Si kitu kidogo ni jambo la kujivunia kwa Watanzania.

Ali Kiba alikutana na wachezaji wa Yanga kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam na kwa pamoja wakapiga picha kwa furaha.

KIba akitokea Afrika Kusini ambako aliingia mkataba huo na Yanga wakitokea Angola ambako walifanikiwa kusonga mbele licha ya figisu kibao walizofanyiwa.


Hii ndiyo Tanzania tunayoitaka, Tanzania ya mapambano kwa ajili ya mafanikio. Lazima tukubali walichokipata Yanga hakikuwa kitu rahisi kukifikia, ilikuwa kazi ngumu iliyohitaji moyo wa uvumilivu na unaotaka ushindi.

Kiba pia, kupata mkataba wa Sony ambayo inaingia mikataba na akina Beyonce na wasanii wengi wakubwa, pia si jambo la kuliona ni dogo sana.

Huenda kwa upande wa burudani tumfanye Kiba kuwa changamoto, mfano wa kuigwa na watu wamuone sehemu ya mafunzo. Wapambane ili kupata mafanikio binafsi ambayo yatageuka kuwa mfano kwa Taifa.

Kwa Yanga, hakika wamefanya kazi kubwa. Kama utakataa itakuwa ni kujirudisha nyuma mwenyewe. Kinachotakiwa ni kuwapongeza na kuwachukulia kama mfano na changamoto ya kuyakimbiza mafanikio.

Ila angalizo kwa upande wa Yanga na Ali Kiba, kila walichokipata si mwisho wa mafanikio wasije wakavuta shuka na kulala usingizi wa pono.

Sasa ndiyo alfajiri na mambo yaanza, Yanga wajue wanakwenda kukutana na timu zenye kiwango cha juu kabisa kisoka.

Kiba lazima ajue, Sony ni watu makini na wanataka kazi hasa ya kiwango cha kimataifa. Hivyo lazima apambane na kuzidisha ubora ili kuonyesha kwamba hawakukosea na ikiwezekana waongeze maslahi zaidi naye aendelee kuitangaza Tanzania kimataifa.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic