May 21, 2016Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, amesema hatakuwa tayari kupokea ofa ya Klabu ya Golden Arrows ya Afrika Kusini kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wao, Ibrahim Ajib.

Poppe amesema hayo huku kukiwa na taarifa kuwa, Ajib amefuzu majaribio yake katika Klabu ya Golden Arrows na kilichobaki ni timu hizo kukubaliana kuhusu usajili tu.

Poppe alionyesha kukerwa na kitendo cha Ajib kuondoka Simba bila ya kuaga kwenda Afrika Kusini kufanya majaribio Golden Arrows inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini.

Ajib aliondoka nchini na anayetambulika kama meneja wake, Juma Ndambile huku kukiwa na sintofahamu ya mkataba wake, mwenyewe alidai umeisha lakini Simba wanakataa. 

“Hiyo ofa binafsi siihitaji, wanaweza kuijadili na wakala wake kama alivyoondoka hapa. Hii maana yake ni sawa na mtu amejaribu kukuibia halafu kashindwa, sasa anakuja kukuomba umpe alichohitaji, siyo sawa.

“Hatujui tumchukulie hatua gani Ajib lakini tukishakaa na kujadili tutajua inakuwaje kuhusiana na masuala yake yote. Lakini najaribu kumuangalia hata huyu meneja wake, anafahamika kuwa ni mtu wa Simba na kuna kipindi aliwahi kupewa cheo.

"Sasa inakuwaje anadanganywa na mchezaji naye anakubali tu? “Alishindwa nini kuja kuhakikisha kuhusu mkataba wa Ajib mpaka akaamua kuchukua uamuzi wa kuondoka naye bila ruhusa? Na hao Golden Arrows inakuwaje wanazungumza na mchezaji mwenye mkataba kamili timu nyingine?” alihoji Hans Poppe.


Alisema moja kati ya hatua watakazochukua ni kuandika barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Chama cha Soka Afrika Kusini (Safa) kuhusu kitendo cha meneja huyo, Ajib na Golden Arrows kuwasiliana bila ruhusa ya Simba.

1 COMMENTS:

  1. Kwahiyo inaonekana Hans Pope ndiye kiongozi wa juu wa simba maana kila kukicha ni yeye tuu anayesemea mambo yao!Aveva vipi kaka?!

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV