May 21, 2016

CHANONGO WAKATI AKIWA SIMBA...
Kufikia katika makubaliano na kiungo mshambuliaji wa Coastal Union, Juma Mahadhi kwenye kikosi cha Yanga, kumezuia usajili wa nyota wa Stand United, Haruna Chanongo katika kikosi hicho cha mabingwa wa Ligi Kuu Bara.

Chanongo ni miongoni mwa wachezaji waliokuwepo kwenye orodha ya wachezaji waliotakiwa kusajiliwa Yanga kwa jili ya msimu ujao ili kumpa ushindani winga Simon Msuva katika namba saba.

Mahadhi ambaye ni mpwa wake Waziri Mahadhi ‘Mendieta’, aliyewahi kuichezea Yanga, amefikia makubaliano na Yanga, na atamwagiwa Sh milioni 30 kwa ajili ya mkataba mpya.

Mmoja wa watu muhimu katika benchi la ufundi la Yanga, amesema mazungumzo na Chanongo yalianza tangu msimu uliopita kwa ajili ya kumsajili, lakini yamefutwa baada ya kumpata Mahadhi.

“Tunaamini tumempata mchezaji sahihi tuliyekuwa tunamhitaji ambaye aina yake ya uchezaji ya kasi na kufunga haitofautiani na Chanongo, hivyo (Chanongo) tumemuondoa kwenye usajili wetu.

“Katika usajili huu, tunaongeza wachezaji wachache wazawa kutokana na ubora wa kikosi chetu kilichofuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

“Kocha (Hans van Der Pluijm) alitupa pendekezo la kusajili kiungo wa pembeni namba saba mwenye uwezo wa kumpa changamoto Msuva, ndiyo maana tumemsajili Mahadhi,” kilisema chanzo hicho.


Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro akizungumzia usajili huo, alisema: “Muda wa kulizungumzia hilo suala bado haujafika.” Kwa upande wake, meneja wa Chanongo, Jamal Kasongo alisema: “Sina taarifa hizo, ila kama kuna timu inamtaka watoe Sh milioni 25.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV