May 16, 2016


Na Saleh Ally
BAADA ya uongozi wa Yanga kutangaza kumfuta kazi aliyekuwa Katibu Mkuu, Dk Jonas Tiboroha, baadhi ya mashabiki Yanga walianzisha figisu wakidai yeye ndiye injini ya klabu hiyo, hivyo wanataka arudishwe.

Waliamini kuondoka kwake, Yanga ingefeli na mambo yangeenda kombo. Lakini haikuwa hivyo, mwisho Yanga imechukua ubingwa wa Tanzania Bara ikiwa ina mechi tatu mkononi, wakati ilifanya hivyo msimu uliopita ikiwa na mechi mbili mkononi.

Waliokuwa wakipiga kelele wakati huo kuhusiana na Dk Tiboroha, leo hawawezi kufungua tena mdomo na kulalama. Maana Yanga ina mafanikio zaidi na sasa inapigania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, ngoma itakuwa keshokutwa.

Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Mehbub Manji, huenda ndiye wanapaswa kuwa na hofu naye kama akiondoka leo. Lakini pia wanaweza wasiwe na hofu kama watapata mtu sahihi wa kuendesha mfumo.

Ambacho kinaifanya Yanga iwe imara katika kipindi hiki zaidi ni mfumo, ingawa aliyesaidia kuusimamisha ni Manji ambaye kama ataondoka, kiongozi atakayefuatia anatakiwa kuwa imara kweli kuusimamia, la sivyo Yanga itayumba kwa kiasi kikubwa kupita kiasi na huenda utakuwa wakati mgumu kuliko wowote uliowahi kutokea.


Tofauti:
Kipindi hiki ndicho ambacho Simba wana wakati mgumu sana. Mashabiki wake wanateseka nafsi, masikio, macho na sasa hawana amani kabisa kwa kuwa kila jina baya ni lao na watani wao wanawabandika.

Asikudanganye mtu kwamba viongozi wa Simba hawafanyi kazi au hawaipendi Simba, au hawajitumi au ni watu wabaya. Wao wamezidiwa nguvu na mfumo wa Yanga ambao unasimamiwa na mtu mmoja tu anayewaamini watendaji wake.

Manji ana akili sana, achana na habari za mitaani. Ni mtu anayejua nini anachokifanya. Huenda amechukua nusu ya robo ya mfumo namna anavyoweza kuendesha makampuni yake makubwa na kuuingiza Yanga. Sasa utaona kila kitu kinakwenda kikiwa kimenyooka. 

Sijui Yanga wanapataje fedha zao, sitaki kuingia huko. Lakini nataka nikueleze tofauti yao na utendaji wa Simba ambao ni wa kizamani sana na lazima wabadilike.


Kama Simba wataendelea wanavyofanya sasa, Yanga ikaendelea kuwa hivi chini ya Manji, basi Simba watarajie vilio sasa, baadaye, kesho na ikiwezekana wakati wote.
Kila kitu cha Yanga sasa kinakwenda kwa mfumo sahihi wa ofisi na hauwezi kuingiliwa. Viongozi wawili wa juu Manji na makamu wake, Clement Sanga ndiyo wanaoshikilia mfumo huo ufanye kazi.

Ukiangalia aina ya utendaji wa Sanga pia utaona, si mtu mwenye makuu, mwadilifu na anayetaka mambo yaende kwenye mstari na uhakika.

Vitu vya ofisi vinapita kwenye usahihi. Hesabu za fedha, zinakaguliwa kila mara na kila fedha inayotakiwa kutoka, lazima ipitishwe na wakubwa hao wa juu. Hawajapitisha, haitoki. Sababu za kutaka kuitoa hazijitoshelezi, haitoki.

Hivyo, ndani ya Yanga, inawezekana kukwapua fedha kirahisi, inaweza kuwa sawa na ngamia kupita kwenye tundu la sindano. Kila mmoja ana hofu na fedha za klabu, hii inasaidia kila senti ya klabu kwenda kwenye malengo kwa ajili ya manufaa ya Yanga na si vinginevyo.


Mkubwa:
Hakuna mkubwa ndani ya Yanga zaidi ya klabu. Hakuna kocha wala mchezaji ambaye yuko juu ya klabu. Kama haukubali hili, nakuuliza umewahi kusikia mchezaji Yanga amegoma? Je, unadhani wao hawajawahi kucheleweshewa mshahara?

Umewahi kusikia mchezaji anabishana na meneja au kuingia kwenye mzozo kama ule wa meneja wa Simba, Abbas Ally ‘Gazza’ na Hamisi Kiiza unatokea Yanga? Sahau na hakuna nafasi.

Nidhamu:
Nidhamu ya Klabu ya Yanga iko juu sana. Pamoja na Manji kuwa juu, lakini ametengeneza mfumo unaowafanya viongozi wa klabu hiyo waheshimike sana na wachezaji pia waheshimiane.

Mfano mzuri, Kocha Mkuu Hans van Der Pluijm. Huyu ndiye bosi wa benchi la ufundi na ndiye mwenye maamuzi ya mwisho kuhusu wachezaji.


Nakuhakikishia, kila mchezaji anayesajiliwa lazima Pluijm akubali, akikataa mchezaji hana nafasi. Simba hili lina utata, inawezekana kiongozi mmoja au wawili wenye ushawishi wakamsajili mchezaji. Au kocha akamtaka mchezaji fulani na akaambiwa hapana. Inawezekana pia kiongozi mmoja akawa anawajua wachezaji kuliko kocha.

Manji alichofanya, kocha kaachiwa aanguke na zigo lake. Yeye aseme anataka wachezaji katika nafasi gani, wakitafutwa au akiwaleta auhakikishie uongozi anawataka. Mwisho wanasajiliwa na wakiboronga, atakuwa na cha kujibu.

Kumpata:
Kumfikia Manji ni vigumu sana. Nina imani haujawahi kumuona akimsajili mchezaji yeyote, hiyo ni kazi ya kocha na mara nyingi kazi zake hufanywa na makamu wake, Sanga ambaye anajulikana ni mtu asiyependa mzaha na asiye mwoga wala kinyongo.

Hofu:
Ndani ya Yanga kuna hofu, Watanzania wengi au binadamu wengi tunaongozwa na hofu, usikatae.
Wengi wanapokuwa hawana hofu huboronga, lakini ikiwepo wanakuwa makini na kufanya kazi kwa juhudi na mafanikio yanapatikana.

Hata Donald Ngoma, akileta usupastaa ‘nyaunyau’ nakuhakikishia ataondoka Yanga halafu atatafutwa mkali zaidi yake ili afanye kazi bora.

Kila mmoja hana uhakika wa kubaki Yanga kama ataboronga au kuharibu katika kitengo chake. Kila mmoja anajua Yanga inataka kilicho bora zaidi, kama hauna, basi nafasi hauna.
Hivyo watendaji wa juu wa Yanga, makocha na wachezaji, kila mmoja anajituma kwa kuwa anajua akifanya kosa, safari imemkuta.

Angalia Simba, leo wachezaji wanatoroka kwa kuwa hawana hofu. Yanga kila mmoja anajua nini cha kufanya ili apate ruhusa. Ndani ya Yanga, kikubwa kuliko vyote si kiongozi, kocha wala wachezaji, ni klabu yenyewe.

Ndani ya Yanga, mfumo ndiyo kila kitu. Kikubwa sasa ni kiongozi wa kuushikilia. Ukiendelea kufanya kazi hivyo, Yanga hakutakuwa na wa kuizuia. Lakini mfumo ukiyumba, hata Yanga itaanguka kama mtu aliyejikwaa kwenye kisiki wakati anakimbia kwenye kiza.

Simba wanapaswa kutengeneza mfumo utakaoheshimika badala ya heshima kwenda kwa mtu mmojammoja.

2 COMMENTS:

  1. Ila ww si ulikuwa mmoja wapo wanaompigia kampeni Tiboroha?
    Afadhari umejua kuwa hukuwa na mtazamo sahihi juu ya maamuz ya Manji.

    ReplyDelete
  2. Hii Yanga ya bmwaka huu sio mchezo.Imeweza kupata pointi 72 kwa mechi 29 wakati Arsenal,Tottenham,Man City,Man United,Chelsea na Liverpool zimeshindwa kufikisha idadi hiyo ya pointi baada ya kucheza mechi 38.Ynga pia imeshinda mechi 22 kati ya mechi 29 idadi ambayo ni kubwa kuliko mechi walizoshinda aRSENAL,tOTTENHAM,Man City,Man UTD kwa mechi 38

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV