May 21, 2016


Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema litafanyia uchunguzi tuhuma za Yanga kufanyiwa vurugu nchini Angola ilipokuwa ikicheza na Sagrada Esperanca mechi ya kufuzu hatua ya makundi Kombe la Shirikisho.

Yanga imelalamika kufanyiwa vurugu hizo tangu ilipotua nchini humo katika Jiji la Luanda hadi ilipokuwa mjini Dundo, ambapo walihangaishwa katika usafiri na kuibiwa baadhi ya vifaa vyao.

Pia maofisa wa Esperanca waliwazuia waandishi wa habari wa Tanzania kufanya kazi zao ipasavyo ikiwemo kuwakataza kupiga picha na kuketi sehemu zisizostahili kwa kazi zao.


Hata hivyo, Yanga ilifungwa bao 1-0 na kufanikiwa kutinga hatua ya makundi Kombe la Shirikisho kwani katika mchezo wa awali jijini Dar es Salaam ilishinda mabao 2-0. Imefuzu kwa mabao 2-1.

Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa, amesema watakaa na kujadili kile kilichotokea Angola kisha watafanya uchunguzi na kuchukua hatua.

“Kama shirikisho hatukufurahishwa na vitendo walivyofanyiwa Yanga, pia nichukue nafasi hii kuwapongeza kufuatia hatua waliyoifikia,” alisema Mwesigwa.


“Tutakaa na kufanya uchunguzi wa kina juu ya walichofanyiwa Yanga, tukibaini tatizo tutajua tuchukue uamuzi gani juu ya hilo.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV