Wanachama wa Yanga wakiongozwa na Baraza la Wazee la Yanga, wameliomba Jeshi la Polisi Tanzania Kanda ya Ilala kuwaruhusu kufanya maandamano.
Wanachama hao wamefikia uamuzi huo kwa madai kuna njama za magazeti ya Nipashe na The Guardian yanayomilikiwa na Reginald Mengi kumchafua mwenyekiti wao, Yusuf Manji.
Vita hiyo, kati ya wanachama wa Yanga na magazeti hayo inazidi kuchukua kasi baada ya wanachama wa Yanga kuyachoma na kuyachana ikiwa ni ishara ya kuonyesha hasira zao.
Katibu wa Baraza la Wazee Yanga, Ibrahim Akilimali amewasilisha barua kwa Jeshi la Polisi kuomba maandamano hayo.
“Kweli nimefanya hivyo, tumechoka maana wanatusakama sana. Sisi tunataka maandamano ya amani kupinga hili.
“Manji sasa si mkurugenzi wa makampuni yanayotajwa na magazeti hayo. Watuachie afanye kazi za Yanga maana sasa ndiyo tumefuzu kucheza hatua ya robo fainali.
“Wanamchanganya makusudi, tena wanafanya hivi kwa kuwa kipindi hiki Yanga imefuzu ndiyo wameanza kuandika stori zake.
“Mbona hawakuandika kabla Yanga haijafuzu, wanatuchanganya kwa makusudi,” alisema.
Bado haijajulikana kama Jeshi la Polisi litatoa ruhusa kwa wanachama hao kufanya maandamano katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Bado wakuu wa magazeti hayo hawajatoa kauli yoyote kuhusiana na hatua hiyo ya wanachama wa Yanga, hasa uamuzi wa kuyachana na kutyachoma moto.
0 COMMENTS:
Post a Comment