Nyota wawili wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Shomari Kapombe na Pascal Wawa hivi sasa wapo jijini Cape Town, Afrika Kusini kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya zao.
Mabeki hao waliondoka nchini tokea Jumanne iliyopita wakiongozana na Daktari wa Azam FC, Juma Mwimbe, ambapo watafanyiwa vipimo vya afya kwenye Hospitali ya Vincent Pallotti iliyopo jijini humo.
Daktari huyo ameuambia mtandao rasmi wa klabu ya Azam FC kuwa wachezaji hao tayari leo wamekutana na madaktari watakaowafanyia uchunguzi na kesho watachukuliwa vipimo kabla ya kupewa majibu yao juu ya matatizo yanayowakabili.
“Wawa amekuja huku kufanyiwa uchunguzi wa goti lake la kushoto linalomsumbua, kama unavyojua Kapombe yeye alishaanza matibabu ya tatizo lake la Pulmonary Embolism alilopata msimu uliopita.
“Hivyo naye yuko hapa kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi ili kuangalia maendeleo yake baada ya kutumia dawa za awali alizopewa wakati wa mwanzo alipopata tatizo hilo, lakini afya yake inaendelea vizuri kabisa kwa sasa,” alisema.
Wachezaji hao wote walipata matatizo ya kiafya kuelekea mwishoni mwa msimu na kupelekea kukosa mechi zote za Azam FC zilizobakia kwa msimu huo.
Wawa alipata majeraha ya goti dakika za mwisho katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Esperance ya Tunisia, ambao Azam FC ilishinda mabao 2-1 yaliyofungwa na Farid Mussa na Ramadhan Singano ‘Messi’.
Kapombe yeye alipata tatizo hilo la kiafya wakati Azam FC ikiwa mkoani Mwanza kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Toto Africans, ulioisha kwa sare ya bao 1-1, bao la mabingwa hao likifungwa na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ na Wazir Junior akiifungia Toto.
0 COMMENTS:
Post a Comment