June 24, 2016


Uongozi wa Klabu ya Azam umetamka kuwa upo tayari kumuuza mshambuliaji wao, Kipre Tchetche kwenda klabu yoyote ambayo itakuwa tayari kuuvunja mkataba wa mwaka mmoja uliosalia kwa straika huyo katika klabu hiyo.

Kipre amekuwa akihusishwa kutaka kusajiliwa na timu nyingine zikiwemo za nje ya nchi huku Yanga ikiwa moja ya klabu za ndani iliyowahi kutajwa kumuwania.

Ofisa Habari wa timu hiyo, Jaffar Idd alisema kuwa licha ya kwamba mpaka sasa hawajapokea ofa ya mchezaji yeyote wa kikosi chao kutakiwa na timu nyingine lakini hawatakuwa wagumu kuwapiga bei wachezaji hao endapo tu timu ambazo zinawataka zitapeleka ofa ya maana.

“Tunasikia tu kuwa baadhi ya timu zina mpango wa kumsajili Kipre, sisi tunawaambia waje kama kweli wana nia hiyo wala wasiogope waje tujadiliane na kuona jinsi gani wataweza kuvunja mkataba wake uliobakia wa mwaka mmoja kwani sasa bado ni mali yetu.

“Tupo tayari kuona tunamuachia mchezaji yeyote yule kwa timu itakayokuwa inamhitaji lakini tunachotaka ni viongozi wa klabu hizo wafuate mipango yote ya usajili na siyo kufanya vitendo ambavyo siyo vya kimichezo na kama wakitekeleza mambo hayo sisi tutawapa ruksa ya kuondoka,” alisema Jaffar. 


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV