August 31, 2016


NAPE 

Na Saleh Ally
SIKU mbili zilizopita, Kampuni ya Multichoice Tanzania, ilifanya hafla ya kuwapokea wanamichezo waliokwenda kushiriki Michezo ya Olimpiki katika mji wa Rio de Janeiro nchini Brazil.

Katika hafla hiyo kwenye hoteli moja kubwa jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye, alikuwa mgeni rasmi na baadaye alipata nafasi ya kuzungumza.

Kwanza nianze kuwapongeza Multichoice Tanzania pamoja na DStv kutokana na uamuzi wao wa kuwasindikiza wanamichezo hao, pia kuwapokea na wakawapa zawadi licha ya kwamba Tanzania haikufanya vizuri.

Tunajua, katika nchi mbalimbali, mfano Zimbabwe, Rais Robert Mugabe alisema wanamichezo waliokwenda Rio waliboronga na wachukuliwe hatua. Kenya pia viongozi wa Kamati ya Olimpiki wako matatani na wengine wamefikishwa mahakamani kwa uzembe wakati wa maandalizi kabla ya kwenda kwenye Olimpiki.

Waziri Nape alitaka wanamichezo wasivunjwe moyo, naungana naye. Lakini bado nawakumbusha wanamichezo wenyewe, kwamba hatuwezi kuendelea kuwaunga mkono wakati wanaendelea kuboronga, tutawasema tu.

Waziri Nape alieleza kuchukizwa kwake na namna wanahabari wanavyokosoa bila ya kueleza nini kifanyike. Pia ninaungana naye, hapa Championi hatujaguswa na hilo kwa kuwa tunaendelea kukosoa na kuwaambia kipi cha kufanya, leo nitarudia.

Kwamba viongozi wengi ni wabinafsi, wanaingia kwenye michezo kwa ajili ya maslahi yao binafsi, kuna undugu, ubinafsi na hata wengine hufurahia wanaoipata nafasi wawe watoto wa wapenzi au nyumba ndogo zao huku wakiacha wanaostahili kushiriki.

Nilimuona kiongozi mkuu wa chama cha riadha, akizungumza maneno mengi na kuingiza siasa. Kwangu niliamini hao ndiyo watu wanaoangusha michezo kwa kiasi kikubwa. Maneno mengi na hakuna utekelezaji.

Hakuna medali, hatuwalaumu wanariadha na wanamichezo wengine. Lakini bado viongozi wanapaswa kuwajibika katika hilo. Hawapaswi hata kidogo kujificha kwenye kivuli cha maneno ya Waziri Nape ambaye kama mzazi lazima asisitize aliyoyasema, kwamba waungwe mkono.

NAPE AKIWA OFISINI AKIENDELEA NA MAJUKUMU YA KITAIFA.

Lakini, Waziri Nape huyohuyo, alitoa kauli ambayo ninaamini ndiyo wakati mwafaka kwa kuwa ameitoa katika kipindi ambacho inahitajika katika michezo ya nchi yetu. Hii inawagusa kuanzia watu wa riadha, netiboli, mpira wa kikapu, ngumi, soka na michezo mingine.

Waziri Nape alisema, kila kiongozi lazima afanye kazi kwa  mafanikio kwa muda aliopo. Ahakikishe kuwepo kwake kuna tija na akasisitiza suala la viongozi kuacha kuongoza kwa ajili ya maslahi yao binafsi.

Akasisitiza suala la viongozi wengi kuwa kwenye vyama vya michezo huku wakiona ni kama hiari na hata wakiboronga hakuna wa kuwahoji.
Alimalizia kwa kusema hivi: “Kama unaona umeshindwa, hakuna cha maana unachofanya, basi mara moja ondoka, waachie wengine ambao wanaweza.”

Mimi sasa, ninaunga mkono hivi: “Viongozi wababaishaji wa soka, sasa inatosha. Kuanzia kwenye soka, kwenda kwenye mpira wa kikapu, ngumi na michezo mingine. Viongozi wauza maneno na mlio kwenye michezo hiyo ili kuendelea kujulikana, ili kusaidia makabila yenu au mikoa yenu au kutaka baadaye mpate nafasi ya kuingia kwenye siasa, sasa basi imetosha.

“Ondokeni, tafadhali ondokeni muwaachie wanaoweza. Mnailalamikia serikali haisaidii, wakati kuna fedha nyingi mnapata kutoka Fifa, IOC na kwingineko na hazileti maendeleo hata kidogo.

“Viongozi wengine mmefanya vyama vya soka kama mali yenu. Mnaona hakuna wa kuwauliza isipokuwa Fifa au IOC tu. Mmesahau nyie mnawatumikia Watanzania na si mashirikisho hayo ya kimataifa.

“Mnajivisha Umungu mtu wa kutaka muabudiwe au kuonekana hamuwezi kuguswa. Sasa kitanzi hicho cha Waziri Nape mjipime, kama hakuna mlilofanya. Basi nendeni, waachieni Watanzania wengine wenye uchu wa kuleta maendeleo, kwani wapo.

“Nasisitiza, Watanzania wenye uwezo wa kuleta maendeleo wapo. Waziri Nape atafanikiwa kwa namna alivyoanza. Maana watu wa michezo ni wajuaji na vichwa ngumu na wapenda siasa kuliko wanasiasa.

“Sasa kitanzi cha Waziri Nape, kila mtu akipokee mkononi mwake, halafu apime anaonaje au wakati gani anaweza kujivika.


“Wakati anaanza kuyazungumza, alisema yanaweza kuonekana ni ya kidikteta. Mimi namwambia Waziri Nape, wala hakuna udikteta lakini mabadiliko yatapatikana kwa uamuzi kama huo maana watu wa michezo wametuangusha miaka mingi sana kwa kuwa tu wanaelezwa kwa kubembelezwa na wao wamejenga hisia sasa kuwa wanawatumikia Wazungu wa mashirikisho ya nje na ndiyo wenye nguvu ya kuwaambia hapana kama ambavyo TFF inaamini Caf na Fifa ndiyo wakubwa kwake na Watanzania si lolote, inaweza kuamua inavyotaka yenyewe, jambo ambalo si sahihi hata kidogo na ni adui mkubwa wa mabadiliko au maendeleo ya soka ambalo limezidi kudorora kutokana na rundo la uozo.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic