September 2, 2016

KAVUMBAGU (KULIA)...
Straika wa zamani wa Yanga na Azam FC, Mrundi, Didier Kavumbagu ameamua kumueleza ukweli mshambuliaji wa Simba, Mrundi, Laudit Mavugo kuhusiana na kiwango alichonacho na nini cha kufanya kama kweli anataka kufanikiwa katika Ligi Kuu Bara.

Kavumbagu ambaye amecheza mechi kadhaa na Mavugo wakiwa wote timu ya taifa ameanza kwa kueleza kuwa kwa tathmini yake mshambuliaji huyo anamwona ni wa kawaida tofauti na sifa anazozisikia akipewa na watu wengine.

“Mavugo ni straika wa kawaida, siwezi kusema ni hatari sana kama anavyozungumziwa na wengine. Nayasema haya kwa kuwa ninamfahamu tangu tukiwa tunakutana timu ya taifa mpaka anakuja Tanzania.

MAVUGO
“Anapaswa kuelewa kuwa amekuja kwenye ligi ya Tanzania, haitaji mazoezi ya timu pekee na kipaji alichonacho kama kweli anataka kufanikiwa akiwa hapa. Anahitaji kufanya mazoezi ya ziada na awe na nidhamu ya hali ya juu, vinginevyo atasahaulika muda si mrefu.

“Ishu ya kuonekana yeye ni hatari, tayari watu wameshaamini hivyo kwamba yupo vizuri sana, sasa anahitaji kulithibitisha hilo na hilo lipo mikononi mwake, anatakiwa apambane kuonyesha kuwa mashabiki hawakukosea kuamini kuwa ni straika hatari.

“Sitaki kuzungumzia kuhusu ushindani kati yake na Amissi Tambwe (wa Yanga), lakini kwenye timu ya taifa mimi na Tambwe huwa tunaanza kikosi cha kwanza na yeye (Mavugo) anakuwa benchi, sasa kwa hivyo inatosha kufahamu ushindani uliopo mbele yake kwa sababu huwa sipendi kufananisha vitu,” alisema Kavumbagu.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV