Na Saleh Ally
TASNIA ya michezo hapa nyumbani ina matatizo lukuki ambayo yameifanya kuzidi kudorora kila kunapokucha kwa kuwa inakwenda kwa kusuasua sana.
Mwenendo wa michezo kwa maana ya upatikanaji maendeleo umekwama kabisa. Na utaona katika mashirikisho au vyama vya michezo, baadhi ya viongozi ni kama wamejimilikisha na kuwa vyao.
Kitu kibaya zaidi, mfano viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hawataki kuguswa au kuelezwa ukweli. Kila anayewazungumzia kuwakosoa, wangependa aonekane ni mbaya kwa jamii wakati hakuna wanachofanya kwa ajili ya kulenga kusaidia michezo.
Hata vichache wanavyofanya vinakuwa vinatokana na nguvu ya ukosoaji ambayo inawapa hofu, hivyo wanaamua kutafuta kivuli kujikinga mapema ili wasije wakatumbuliwa kwa kuwa serikali ya awamu ya tano, inaonekana haitaki utani.
Hii tabia si ya TFF pekee, hata Chama cha Riadha Tanzania (RT), nao wamejificha kwenye kichaka cha kuonyesha kuwa wanafanya vizuri sana na anayewagusa kuwakosoa ni mtu mbaya na asiyejali mazuri yao ambayo hayaonekani.
Vurugu zipo kila sehemu hasa unapozungumzia michezo. Chama cha Olimpiki Tanzania (TOC) ndiyo hadithi tupu na kuna ambao ni sawa wamejimilikisha eneo hilo na ajabu hawataki kuguswa kabisa, wamegeuza ni kama mali yao na kisingizio ni uzoefu au waliwahi kuleta heshima wakiwa wanamichezo uwanjani. Sasa ni viongozi na hakuna lolote la maana wanalofanya.
Hapa nyumbani, Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ndiyo wasimamizi wakuu wa michezo kwa niaba ya serikali. Lakini niwe mkweli, kwamba hawana msaada wowote kwenye michezo, wamekuwa wakikaa sana ofisini na kuibuka kwa shughuli zaidi za kisiasa kuliko maendeleo ya michezo.
Kama wao ndiyo wasimamizi, wanaweza kujivunia kipi kama ubora wa sehemu ya kazi yao kwa ajili ya kusaidia michezo wakiwa wanaibadilisha kutoka ilipo sasa na kwenda mbele?
Wanaweza kusema lini wamewahi kuisimamia sera na kupambana kuhakikisha kuna utekelezaji? BMT wanajua nini kuhusiana na ukuzwaji wa vipaji kwa ajili ya kuwa na timu bora za michezo?
Kwa nini akina TOC, RT, TFF na wengine wanafanya vyama utafikiri ni mali ya viongozi na mambo yasiyo sahihi ni rundo na wao hawachukui hatua.
BMT imekuwa ni kama ofisi ya ziada ya watu wengine, ipo ilimradi ipo tu na kuna wakati ilikuwa ikichukua asilimia moja katika kila mechi ya Ligi Kuu Bara. Kama hiyo inaendelea, bado ni kosa kubwa maana hakuna faida na hatujui wanaisimamia michezo wapi.
Wakiibuka watakuwa wanazungumzia au kuanzisha mgogoro, wakiibuka BMT kutakuwa na timu inasafiri kucheza michuano ya kimataifa. Watakabidhi bendera, watapata nafasi ya ‘kupiga’ siasa na baada ya hapo, kasi ya mwezi au zaidi itakuwa imepita!
Michezo ni mipango ya muda mfupi na mrefu. Anayekuwa msimamizi wa michezo akiwa hana uwezo wa kujua maandalizi ya maendeleo yanafanyika vipi na badala yake anakuwa anakurupuka kwa ajili ya mambo ya migogoro au kukabidhi bendera, hakika huu ni uozo na hatufai.
Tunajua kabla serikali haikuwa ikijiingiza ndani katika michezo. Hiyo ilikuwa inachangiwa na watendaji wengi wa BMT kukaa tu ofisini na siamini kama kweli hata mishahara wanayolipwa wanaifanyia kazi na kuisaidia michezo kama sehemu ya ajira katika taifa hili.
Siamini kama BMT ina wataalamu wa michezo au watu wanachaguliwa kwa uswahiba. Pia siamini kama wao BMT walivyo tangu walipotokea wanaamini walipofikia wamesimamia na kusaidia michezo kupiga hatua.
Kama kazi yao ni kusimamia tu, faida yake nini kusimamia ambacho hakina maendeleo na wewe ukiwa umejichimbia tu ofisini. Tuache siasa katika michezo, badala yake tuwe watendaji kuisaidia kukua. Siasa ina sehemu zake.
0 COMMENTS:
Post a Comment