Klabu ya Yanga imetangaza ajenda kumi na moja kwa ajili ya mkutano mkuu wa dharura uliopangwa kufanyika Oktoba 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kaunda jijini Dar es Salaam.
Katika ajenda hizo, moja imeeleza kuwa katika hotuba yake, Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, atawataja maadui wa klabu hiyo, huku kukiwa na msisitizo kuna mamluki wa wafanyabiashara wanaofanya mbinu za kuivuruga Yanga.
Pamoja na ajenda nyingine 10, hiyo moja inaonekana kuanza kuwa gumzo kwenye mitandao, hasa kuhusiana na kwamba Manji atawataja maadui hao wa Yanga, ikielezwa wamepania kushusha hadhi ya klabu hiyo ili kuonyesha Manji ameshindwa.
“Kutakuwa na hotuba ya mwenyekiti, maoni na msimamo wake juu ya maazimio ya wanachama na kusema anayoyajua ya siri kuhusu Yanga na adui wa Yanga.
“Pia atafafanua wanaoleta vurugu, baadhi ni mamluki wa wafanyabiashara wenzake walioshindwa kumshinda kwa njia halali na sasa wanaitumia Yanga kama sehemu pekee iliyobaki kumuumiza kupitia mbinu zinazotumika.
“Mbinu hizo ni kuleta vurugu ndani ya Yanga ili kumchafua binafsi ili kushusha hadhi ya klabu,” ilieleza sehemu ya jenda hiyo ya kumi na moja.
Ajenda nyingine zilizotajwa ni pamoja na kupitia dondoo za kikao kilichopita, kuthibitisha wajumbe wa Bodi ya Wadhamini, suala la kukodisha timu na nembo, kumjadili mwenyekiti (Manji) kuhusiana na kampuni inayotaka kukodisha ambayo ni yake na kubaki kwake katika uenyekiti.
Itakuwa ni mgongano wa mawazo, kupitia utendaji wa kamati ya mashindano, kujadiliwa kwa wanachama ambao hawafiki kwenye vikao na wanakosoa kwenye vyombo vya habari tu na kujadili tarehe ya uchaguzi mdogo kujazia nafasi za wajumbe wa kamati ya utendaji.
Yanga iliamua kuitisha mkutano huo wa dharura baada ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza halitambui klabu hiyo kuikodisha timu yake na nembo yake kwa Kampuni ya Yanga Yetu Ltd.
Mkutano huo unasubiriwa kwa hamu, kwani hivi karibuni Manji alionekana kuudhika na kuendelea kusakamwa hadi kufikia kuona ajitoe Yanga. Lakini mwisho akabadili uamuzi na kusema, mkutano huo wa wanachama ndiyo utaamua juu yake kwa kuwa wanachama wengi wamekuwa wakimuunga mkono.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment