Ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar juzi Jumamosi, ulimfanya Kocha wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog kufikia mechi tisa kwenye Ligi Kuu Bara bila kupoteza na amebakiza mechi moja tu kuandikisha rekodi mpya kwenye Mtaa wa Msimbazi.
Ukiachilia mbali rekodi ya Patrick Phiri ya msimu wa 2009/10, aliyeipa ubingwa timu hiyo bila kupoteza, takwimu zinaonyesha tangu afanye hivyo Phiri, ni Abdallah Kibadeni Mputa pekee aliyefanikiwa kuiongoza timu hiyo kwenye mechi 10 za mwanzo bila kupoteza msimu wa 2013/14.
Mputa ambaye kwa sasa ni mshauri mkuu wa benchi la ufundi la timu ya taifa, Taifa Stars, msimu huo akisaidiana na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, waliiwezesha Simba kucheza mechi 10 pasipo kupoteza kabla ya kukumbana na kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Azam iliyokuwa chini ya Stewart Hall.
Iwapo Simba itafanikiwa kupata pointi dhidi ya Mbao FC kwenye mchezo ujao, basi itakuwa ni rekodi ya aina yake kwa Omog kumfikia babu Mputa aliyetimuliwa mwishoni mwa mwaka 2013 na nafasi yake kuchukuliwa na Mcroatia, Zdravko Logarusic.
Licha ya kudaiwa mchezo mmoja, lakini tayari takwimu zinambeba zaidi Omog mbele ya Mputa kwani katika mechi hizo tisa ameshinda michezo saba na sare mbili, dhidi ya JKT Ruvu (0-0) na Yanga (1-1), wakati Mputa kwenye michezo hiyo 10, alifanikiwa kushinda mitano tu na sare tano.
Msimu huo uliotwaliwa na Azam, Simba ilimaliza katika nafasi ya nne na pointi 38. Ilishinda michezo tisa, sare 11 na ilipoteza mechi sita. Ilifunga mabao 41 na kuruhusu mabao 27.
Simba ya Omog ipo kileleni na pointi 23, yaani pointi 15 nyuma ya pointi za jumla ilizovuna msimu wa rekodi ya Mputa, ikiwa imeshinda mechi nane, moja nyuma ya msimu wa Mputa.
0 COMMENTS:
Post a Comment