October 17, 2016


Baada ya kipa Ali Mustapha ‘Barthez’ afungwe bao la kona ya moja kwa moja na Shiza Kichuya katika mchezo wa watani wa jadi Yanga na Simba hivi karibuni hajaonekana tena kwenye lango la Yanga lakini kocha Hans Pluijm amedai bao hilo siyo sababu ya kipa huyo kusotea benchi.

Barthez alifungwa bao la kona iliyopigwa na Kichuya dakika ya 87 na kuingia wavuni moja kwa moja katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa hivi karibuni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya 1-1.

Kipa huyo, tayari amekosa mechi mbili, dhidi ya Mtibwa Jumatano iliyopita iliyomalizika kwa Yanga kushinda 3-1 na dhidi ya Azam FC jana Jumapili.

Pluijm amesema kipa huyo ana matatizo yake binafsi yaliyosababisha awekwe benchi.

Pluijm alisema, mengi yanazungumzwa kuhusiana na kipa huyo baada ya kufungwa bao la kusawazisha la kona lakini yeye ndiye anayejua sababu hasa ni nini.

Aliongeza kuwa, makosa ni sehemu ya mchezo katika soka, hivyo haoni sababu ya Barthez kulalamikiwa sana baada ya kosa hilo.

“Siku zote soka ni mchezo wa makosa, hivyo lile bao alilofungwa Barthez na Kichuya siyo sababu ya mimi kumuondoa kwenye nafasi hiyo na kumchezesha Dida (Deogratius Munishi).

“Barthez nimemuondoa kwenye kikosi cha kwanza kutokana na matatizo yanayomkabili na siyo sababu hilo bao alilofungwa na Kichuya, Barthez bado kipa mwenye uwezo mkubwa.


“Ni vema watu wakalifahamu hilo, kikubwa nafurahia uwezo wa makipa wangu wote watatu nilionao ambao wanaleta changamoto ya ushindani,” alisema Pluijm.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic