MRWANDA |
Kwa kiwango kinachoonyeshwa na mshambuliaji wa Simba, Mrundi, Laudit Mavugo, kimekuwa kikikosolewa na wengi, straika wa zamani wa Yanga, Dan Mrwanda anayekipiga Kagera Sugar kwa sasa, naye amesema Mavugo haendani na presha ya Simba na hiyo itaigharimu timu hiyo pia.
Mrwanda aliyewahi kuichezea Simba pia miaka ya nyuma, ameyaongea hayo mara baada ya kumalizika kwa mechi yao ya juzi dhidi ya Simba waliyopoteza kwa mabao 2-0 ambapo hakusita kumchambua mchezaji huyo na kukimwagia sifa kikosi cha Wekundu hao kwa spidi waliyokuwa nayo.
MAVUGO |
“Kwa ujumla kikosi cha Simba kipo vizuri, hata wanavyocheza wanaelewana na wanastahili kupata ushindi katika mechi zao, kwa upande wetu naweza kusema tulifanya makosa ya kutotengeneza nafasi nyingi na wao walipopata nafasi wakazitumia ipasavyo.
“Kuhusu Mavugo nafikiri kwa kiwango anachoonyesha, anapaswa kuongeza bidii sana, timu ya Simba aliyopo ni timu yenye presha kubwa na inahitaji mchezaji aliyechangamka na mwenye uwezo wa kuendana na presha hiyo lakini yeye naona haendani nayo.
“Kama ataendelea kucheza hivi, sidhani kwa kweli kama atawapa wanachokihitaji Simba na mwisho wa siku itakuwa hatari kwake, aelewe kuwa timu za Simba na Yanga zinahitaji nini kwa mchezaji wakati wote, ukizingatia wamejenga imani kubwa kwake,” alisema Mrwanda, mchezaji wa zamani wa Moro United.
Katika mchezo huo wa juzi, Mavugo aliingia akitokea benchi kuchukua nafasi ya Fredric Blagnon lakini hakufanikiwa kufunga bao lolote na kuendelea kuwa na ukame wa kutofunga kwa mechi tano mfululizo licha ya awali kufunga mabao matatu mfululizo katika mechi tatu za ligi.
0 COMMENTS:
Post a Comment