Aliyekuwa Kocha wa Stand United ya Shinyanga, Patrick Liewig, ametua kwenye ofisi za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) zilizopo Uswisi, ili kudai haki zake baada ya kuvunja mkataba na timu hiyo.
Liewig ambaye kabla ya kuondoka Stand United alikuwa na mgogoro na klabu hiyo, amesema yupo nchini humo kukutana na wakili wake ambaye pia ni mwajiriwa wa Fifa.
Alisema siku yoyote kuanzia sasa atarejea Tanzania kubeba kila kilichokuwa chake na kuondoka moja kwa moja.
Akizungumza kutoka nchini Uswisi jana, Liewig alisema amefikia uamuzi huo ili alipwe haki zake huku akiwa bado na mapenzi na klabu hiyo.
“Kibali changu cha kufanya kazi kimekwisha na klabu haikuwa na msaada wowote wa kushughulikia kibali kipya, nikaamua kuondoka kwa sababu niliona viongozi hawakuwa wakiiheshimu kazi yangu.
“Sasa hivi nipo Uswisi, nimekutana na wakili wangu kuweka mambo sawa. Nikikamilisha kila kitu nitarejea Tanzania kuchukua kila kilichokuwa changu ili niachane nao kwa amani,” alisema Liewig.
Ofisa Habari wa Stand United, Deokaji Makomba, alikiri kwamba Liewig anadai mishahara ya miezi miwili, lakini kwa sasa hawana uwezo wa kumlipa kwani mdhamini wao Kampuni ya Madini ya Acacia imejiweka pembeni na tayari walishazungumza na kocha huyo kuhusu hali hiyo.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment