October 17, 2016Wiki iliyopita, Kocha wa Stand United, Patrick Liewig alidaiwa kutoweka klabuni hapo kwa kile alichoeleza hakupewa stahiki zake, lakini uongozi wa kikosi hicho umesema licha ya mkataba wake kuwa hai hauna muda wa kumtafuta wala kumlipa kiasi cha milioni 30 walizokuwa wamekubaliana. 

Kocha huyo wa zamani wa Simba, ilielezwa kutokubali kuvumilia hali ya ukata unaoiandama klabu hiyo kwa sasa, ikiwemo kutolipwa sitahiki zake pamoja na wachezaji, tuhuma zilizopanguliwa na msemaji wao, Deokaji Makomba, ambaye amesema kutoroka kwake amejifukuzisha kazi kwa mujibu wa sheria za kimkataba.

Inaelezwa baada ya mchezo wao ugenini dhidi ya Mbeya City, alikatiwa tiketi ya ndege kwenda Mwanza ambako angechukuliwa na gari kwenda Shinyanga, lakini ajabu hakwenda ‘ruti’ hiyo mpaka sasa akiwa hajaonekana kwao.

Katika mahojiano, Makomba amesema kutokana na ukata walionao kwa sasa baada ya Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Acacia kujitoa kuwadhamini, waliketi chini na Mfaransa huyo wakitaka kusaini mkataba mwingine kutokana na kutokuwa na uwezo wa kumlipa kile alichokuwa akilipwa na Acacia, lakini akataa.

“Ukweli ni kwamba kwa sasa hali ya kiuchumi siyo nzuri tangu wajiondoe Acacia. Yeye alikuwa akilipwa na Acacia karibu milioni 15, tulimueleza ukweli kuwa tusingeweza kumlipa kiasi hicho, tukamwambia kama atakuwa tayari, basi asaini mkataba mwingine tunaoweza kuumudu, lakini akakataa.

“Maazimio ya mwisho tulikubaliana apewe mshahara wake wa miezi miwili (Sh milioni 30) ili aondoke lakini ajabu hata kabla ya kile tulichokubaliana akatoroka na atakuwa amepoteza haki zake zote za msingi ikiwemo fedha hizo tulizokuwa tumekubaliana,” alisema Makomba.

Pamoja na ukata wao, lakini uwanjani Stand imeendelea kuwa moto wa gesi ikiwa kwenye nafasi ya pili. Hajapoteza mchezo wowote katika michezo tisa iliyocheza. 
Makomba anasema kwa sasa timu itaendelea kuwa chini ya kocha msaidizi, Athumani Bilal ‘Bilo’.0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV