October 21, 2016

KESSY
Na Saleh Ally
HARUFU ya ushabiki katika suala la kijana Hassan Kessy inazidi kuwa juu kuliko kawaida na wengi wasioelewa, wanaligeuza ni sehemu ya kuonyesha wanaonewa, wananyanyaswa au vinginevyo.
Kessy amejiunga na Yanga akitokea Simba, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ndiyo inayosikiliza kesi hiyo na ilifikia maamuzi kadhaa. Moja ilikuwa ni kumruhusu Kessy kuendelea kucheza kwa ajili ya kuokoa kipaji chake.
Pili ikaamua kuendelea kusikiliza kesi hiyo hadi ilipoipatia uamuzi, tayari ina majibu. Lakini kabla ya kuyatoa, imewataka Simba ambao ni walalamikaji na Yanga ambao ni walalamikiwa kukutana na kulimaliza kirafiki suala hilo.
Wakati hilo linaendelea, juzi Championi Jumatano liliandika kuhusiana na Yanga ambavyo inaweza kupoteza pointi nne kama itashindwa kesi ya Kessy kwa kichwa cha habari kisemacho: “Yanga kupokwa pointi nne”.

Ndani ya ile habari, inaeleza mambo yote ikiwemo Kessy kuruhusiwa kucheza, tahadhari ya Yanga kuacha kumtumia kwa mechi kadhaa na uamuzi wa kamati kuzitaka Yanga na Simba kukutana na kulimaliza suala hilo.

Watu wengi walipiga simu kutaka kupata ufafanuzi, hasa baada ya kumuona Kessy amepangwa katika mechi ya juzi dhidi ya Toto African.

Wengi waliopiga, walionekana husoma lakini hawaelewi, walionekana walisoma mioyo yao ikiwa imezungukwa na mioyo ya hasira ambazo hazina msingi na hawakuelewa, hivyo wakajikuta maswali mengi anayouliza yameelezwa ndani ya habari hiyo.

Wengine ni wale wenye tabia ya kusoma vichwa vya habari na hapo wanaanza kujadili. Habari inaeleza kwa nini Yanga inaweza kupoteza pointi hizo kwa kuwa kesi imeonekana ni ngumu kwao na huo ndiyo ukweli.

Simba sasa nao wanalalamika, kwamba inaonekana TFF wanataka kuipendelea Yanga na ndiyo maana inamchezesha Kessy. Kabla, wako watu wa Simba walipiga kulalamika kwamba kutoa habari ya Kessy ni kuishitua Yanga na hili gazeti ni la Yanga, hivyo tunaitetea kijanja ili isiharibu zaidi.

Ushabiki huu wa hovyo haufai hata kidogo, pia ni vizuri kuacha tukafanya kazi yetu kama chombo cha habari. Watu wanaweza kuwa na ushabiki, waandishi nao ni binadamu, kuna sehemu za kushabikia lakini si kazini au wakati wa kazi.

Suala la Kessy linavyokwenda, utagundua kuna uzembe mwingi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ni sehemu kubwa ya uzembe huo, huenda wangetaka kujisafisha, nitakueleza. Wanajua walitoa leseni na wakashughulikia mchakato wa kibali cha Kessy kwenye Shirikisho la Soka Afrika (Caf), bila ya kuangalia mkataba wake na Simba ukoje.

Mwisho kumekuwa na mabadiliko ya mkataba na ule wa chini ya Juni 15, ukaja wa Juni 20, lakini ndani ya Caf, imeshindikana kubadilisha mambo. Huenda TFF ingefurahia kuona inaonekana hakuna kosa, ili isionekane ni sehemu ya kosa.

Simba pia, itafurahia kuona Yanga ina kosa ili ipate nafasi ya kuikomoa Yanga na Kessy, jambo ambalo si jema na si la kimichezo. Hakuna haja ya kuwekeana visasi hata kama Kessy alikosea au Yanga awali walikataa kukaa na Simba.

Kuna figisu, au fitna za kijinga ambazo hazina sababu wala mashiko zinaendelea. Vizuri Yanga na Simba wakaonyesha ukomavu, waliokosewa na Kessy waamini ni kijana wao na wamsadie na kama Simba watafikia hatua ya kusema wanahitaji malipo, basi waangalie si kukomoa ili Yanga walipe na Kessy acheze.

Vitu viko wazi sana, haihitaji kupindishwa au watu kulilia kama wanaonewa sana. Mashabiki wa Yanga au Simba wasiolijua undani wa suala hilo, pia wanapaswa kujifunza na kutuliza akili wakati wanasoma mambo kuliko kuona kulialia au kulalamika sana ndiyo lugha bora ya ufahamu wa mambo.

Sifa za kuonekana unasema sana kijiweni, zinaweza kuwa bora sana kama ukijaribu kuongeza uelewa wa kila jambo unalotaka kulizungumzia. Siasa biabia, (yaani siasa za kubabaisha), hazina nafasi kwenye hali halisi zaidi ni kupoteza muda tu!

Makubaliano ni Mjumbe wa Heshima wa Caf, Said El Maamry awe msuluhishi. Baada ya gazeti hili kutoa habari ya Kessy, ndiyo TFF ikamtafuta na yeye amekubali. Hii ni habari njema kwa Yanga, Simba na Kessy mwenyewe. Itakuwa bora pia El Maamry akipewa heshima na klabu hizo mbili zimtumie kulimaliza suala hilo kwa kuwa pamoja na ufahamu wa juu wa masuala ya Caf, yeye ni mmoja wa wanasheria wakongwe kabisa hapa nchini.

Wakati mwingine vizuri tukijifunza, kama tunataka kufanya mambo bora, vizuri kujifunza au kusikiliza, kusema tu bila ya kujua unachokizungumza, ni hatari kwa matokeo ya baadaye.

Hili suala halishughulikiwi kwa kasi sahihi, TFF ililiacha tu, kuandikwa kumelichangamsha tena. Nisisitize, kama Yanga ikishindwa bado haikwepi kupoteza pointi kama imemtumia beki huyo. 

Hivyo, vizuri TFF ikaliharakisha pia ili Yanga iwe na uhakika zaidi inapomtumia beki huyo, kuliko kumtumia mara kumuacha kama ambavyo imekuwa ikifanya kwa kuwa haikuwa na uhakika.



3 COMMENTS:

  1. Tunao kujua wala hutupi shida tunajua we ni mnazi wa kutupwa wa Simba hata gazeti lako unaloliandikia nilisha acha kusoma siku nyingi unaleta utetezi leo baada ya Yanga kumchezesha Kessy ulikuwa wapi siku zote toka umeiandika hiyo habari na vipu ile habari uliyoandika "Manji ajitoa Yanga" nayo hujaikanusha acha kutuchezea akili.

    ReplyDelete
  2. mm nadhan sheria ziko wazi haya mambo ya kumalizana pembeni ndyo yanafuga ugonjwa, kama Yanga walifuata taratibu zote na nina iman wanazijua hakuna haja ya vikao vya usuluhishi kessy aidhinishwe kuchezea Yanga na kama hawakufuata utaratibu sheria pia ifuate mkondo wake ili iwe funzo kwake na watu wengine isiwe watu wanataka suluhu kwasababu ni Yanga na simba hapana tumeona ulaya barcelona wamechukuliwa hatua, juve walishushwa daraja sidhan kama simba na yanga ni kubwa kuliko hizo timu so sheria ifuate mkondo haya mambo ya suluhu suluhu ndyo yanalea maradhi

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic